Mar 14, 2022 08:13 UTC
  • Macron na Biden waafikiana kuongeza vikwazo dhidi ya Russia

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amezungumza kwa njia ya simu na mwenzake wa Marekani kuhusu mashambulio ya Russia dhidi ya Ukraine, na pande hizo mbili zimekubaliana kuzidisha vikwazo dhidi ya Moscow.

Marais hao wamejadiliana kuhusu mashauriano ya kidiplomasia ya karibuni na kusisitiza juu ya dhamira yao ya kuiwajibisha Russia kutokana na uvamizi wake huko Ukraine na wakati huo huo kutangaza wazi uungaji mkono wao wa kila upande kwa serikali ya Kyiv.

Kwa mujibu wa ripoti, Macron katika mazungumzo yake ya simu na Rais Volodymyr Zelinsky wa Ukraine  aliashiria hali ya Ukraine na kuelezea uungaji mkono wake kamili kwa Kiev na kuelezea juu ya msaada wa ziada wa EU kwa Ukraine. Pia walibadilishana mawazo kuhusu kuendelea kwa mazungumzo kati ya Russia na Ukraine.  

Rais wa Russia, Vladimir Putin Alhamisi tarehe 24 Februari aliamuru operesheni maalumu ya kijeshi katika eneo la Donbass kujibu ombi la msaada wa kijeshi kutoka kwa viongozi wa jamhuri za Donetsk na Luhansk huko Mashariki mwa Ukraine. 

Rais Vladimir Putin wa Russia 

Russia imekuwa ikilalamika kwa muda mrefu kuwa, serikali yenye misimamo ya Kimagharibi ya Ukraine inalenga kujiunga na muungano wa kijeshi wa NATO unaoongozwa na Marekani na hilo ni tishio kubwa kwake. Hivi sasa Russia inasisitiza kuwa Ukraine inapaswa kupokonywa silaha na iwe nchi isiyofungamana na siasa za upande wowote.

Tags