Mar 17, 2022 08:52 UTC
  • Shirika la Afya Duniani laonya kuhusu mlipuko mpya wa corona

Shirika la Afya Duniani limeonya kwamba kuondoa vizuizi vya kijamii, kupunguza uzingatiaji wa masuala ya afya ya umma na viwango vya chini vya chanjo vimesababisha ongezeko la idadi ya visa vya maambukizi ya Covid-19 duniani.

Baada ya mwezi mmoja wa kupungua kwa maambukizi ya corona duniani kote, idadi ya wagonjwa imeongezeka tena katika siku za hivi karibuni, huku China na baadhi ya nchi za Asia zikiweka karantini na vikwazo vya kijamii ili kudhibiti maambukizi hayo.

Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa, kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), virusi vya Omicron aina ya BA.2 vinavyosambaa kwa kasi kubwa, kuondolewa kwa vizuizi vya kijamii na kupunguzwa kwa uangalizi wa masuala ya afya ya umma kunahusika katika kuibuka tena kwa maambukizi ya corona.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema, kunashuhudiwa ongezeko la maambukizi katika baadhi ya nchi, na hii inaonyesha kwamba, takwimu za maambukizi ya virusi hivyo zinazotolewa zinaonyesha sehemu ndogo tu ya hali halisi ya maambukizi ya virusi hivyo.

Image Caption

Maafisa wa WHO wanasema: Viwango vya chini vya kutoa chanjo kutokana na taarifa nyingi za uongo katika baadhi ya nchi pia vimekuwa sababu ya kasi kubwa na mlipuko mpya wa virusi vya corona.

Takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya watu milioni 464,489,108 wameambukizwa virusi vya corona kote duniani na watu wasiopungua 6,081,450 miongoni mwao wameaga dunia kutokana na virusi hivyo. 

Tags