Mar 19, 2022 06:05 UTC
  • Ziara isiyo na tija ya Waziri Mkuu wa Uingereza katika nchi za Saudia na Imarati

Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson mbaye alikuwa ziarani katika nchi za Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), amejaribu sana kuzishawishi nchi hizo mbili ziongeze kiwango chao cha uzalishaji mafuta, lakini amerejea London mikono mitupu.

Katika mazungumzo yake na Mohammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia, Johnson aliitaka Riyadh iongeze idadi ya mapipa ya mafuta inayozalisha kwa siku lakini hakufanikiwa licha ya kudai kuwa safari yake hiyo imezaa matunda mazuri. Alipoulizwa na waandishi wa habari kwamba je, ameweza kumshawishi Bin Salman aongeze uzalishaji mafuta, Johson amesema, msiniulize mimi, kaiulizeni serikali ya Saudia. Lengo la Boris Johnson ni kudhibiti bei ya mafuta nchini Uingereza, kukabiliana na mfumuko wa bei, kusaidia watu wenye kipato cha chini na wanunuzi wa mafuta katika vituo vya kujazia mafuta huko Uingereza n.k, lakini inaonekana mrithi wa ufalme wa Saudia amekataa kuongeza uzalishaji wa mafuta.

Baada ya Russia kuanzisha vita dhidi ya Ukraine, nchi za kambi ya Magharibi zimeanzisha vita vikubwa vya pande zote vya vikwazo na mashinikizo dhidi ya Russia. Vita hivyo vimesababisha matatizo mengi ya kiuchumi, kibiashara na kisiasa na kufika hata kuwekewa vikwazo vyombo vya habari na sekta ya michezo ya Russia. Hata hivyo Marekani na nchi za Ulaya zinatofautiana sana kuhusu suala la vikwazo. Tarehe 9 mwezi huu wa Machi, rais wa Marekani, Joe Biden alitoa amri  ya kupigwa marufuku uingizaji wa mafuta, gesi na bidhaa nyingine za nishati kutoka Russia. Viongozi wa Washington walidai kuwa matatizo yanayotokana na kupanda gharama za uchukuzi nchini Marekani inabidi yavumiliwe kwani ni kwa ajili ya kukabiliana na kile walichosema ni siasa za kupenda makuu za Russia. Hata hivyo uamuzi huo wa Marekani haukuufurahisha Umoja wa Ulaya na Brussels imeupinga hadharani. Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya alisema kuhusu uamuzi huo wa Joe Biden wa kuiwekea vikwazo sekta ya mafuta na gesi ya Russia kwamba, Ulaya haiwezi kuifuata Marekani katika suala hilo.

Joe Biden, rais wa Marekani

 

Pamoja na hayo, Uingereza ambayo imejitoa kwenye Umoja wa Ulaya na hivi sasa inachukua maamuzi kivyake; ya siasa za kigeni na sera za nishati; imeamua kufuata mkumbo wa Marekani katika kuiwekea vikwazo vya nishati Russia. Serikali ya Uingereza imesema kuwa itaacha kuingiza mafuta, gesi na bidhaa nyingine za nishati kutoka Russia kuanzia mwishoni mwa mwaka huu wa 2022. Lakini vikwazo hivyo ni upanga wa ncha mbili. Vina madhara makubwa sana pia kwa Marekani na Uingereza. Gazeti la Daily Mirror la Uingereza limesisitiza kuwa, mashambulio ya Russia dhidi ya Ukraine vimewatia kwenye matatizo makubwa wananchi wa Uingereza. Kila lita moja ya mafuta nchini Uingereza imefikia pence 208 tena katika mazingira ambayo hata kabla ya mgogoro huo, wananchi wa Uingereza walikuwa na matatizo na shida katika kukabiliana na gharama za maisha. Sasa hivi wananchi wa nchi hiyo wa Ulaya wamezidi kuwa chini ya mashinikizo huku bei ikiwa inapanda kila siku katika vituo vya kujaza mafuta kutokana na vita vya Ukraine. Kama tulivyotangulia kusema, vikwazo vya nchi za Magharibi dhidi ya Russia ni upanga wa ncha mbili na vina madhara makubwa pia kwa uchumi wa nchi Ulaya na Marekani 

Sasa hivi Marekani na Uingereza zinazishinikiza nchi za Kiarabu kuongeza kiwango cha uzalishaji mafuta ili kuzuia wimbi la kupanda bei ya bidhaa hiyo muhimu na kupunguza madhara ya vikwazo vyao dhidi ya Russia. Serikali ya Biden huko Marekani imeitaka waziwazi Saudia iongeze uzalishaji wa mafuta. Hata hivyo, baada ya Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) kuona jinsi nchi za Magharibi hasa Marekani zilivyozitelekeza Afghanistan na Ukraine, zimepoteza imani yao kwa nchi hizo. Nchi hizo haziko tayari kuvunja mkataba wao na Moscow unaohusiana na OPEC+ wa kuongeza mapipa 400 tu ya mafuta kila siku. Ni kwa sababu hiyo ndio maana licha ya waziri mkuu mwenyewe wa Uingereza kuzitembelea Saudia na Imarati, lakini amerejea London mikono mitupu. Keir Starmer, mkuu wa chama cha Leba cha Uingereza anasema: waziri mkuu wa Uingereza amekwenda na pipa tupu kuomba mafuta kwa madikteta.

 

Vikwazo dhidi ya Russia vimepandisha bei ya mafuta kwa nchi za Magharibi kama Uingereza na Marekani

 

Naye Masoud Shajareh, Mkuu wa Kamati ya Haki za Binadaamu ya Kiislamu anasema: Kwa upande mmoja, Uingereza inauunga mkono utawala wa kiimla wa Saudia na muungano unaoendelea kufanya jinai na mashambulizi dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Yemen, lakini kwa upande wa pili imechukua msimamo mkali kuhusu russia katika vita vya Ukraine. Ziara ya waziri mkuu wa Uingereza nchini Saudia ni uungaji mkono wa wazi kabisa wa uvamizi na uvunjaji wa haki za binadamu unaofanywa na ukoo wa Aal Saud, dhidi ya Yemen.

Si hayo tu, lakini pia ni Uingereza hiyo hiyo ndiyo ambayo iko bega kwa bega na Marekani katika kuzisingizia nchi nyingine kuwa zinavunja haki za binadamu kutokana na nchi hizo kuwa na misimamo huru na kutokubali kuburuzwa na madola ya kiistikbari wakati wavunjaji wakuu wa haki za binadamu ni madola hayo hayo ya kibeberu.

Tags