Mar 23, 2022 07:28 UTC
  • Taliban yafanya kikao muhimu kujadili mabadiliko serikalini na kutambuliwa kimataifa

Kundi la Taliban nchini Afghanistan limefanya kikao muhimu cha kujadili mabadiliko ya baraza lake la mawaziri na nini kifanyike ili serikali ya kundi hilo itambuliwe na kukubaliwa kimataifa.

Baada ya kupita miezi saba tangu kundi la Taliban liingie madarakani nchini Afghanistan na kuunda serikali ya muda, hadi sasa hakuna nchi yoyote iliyotangaza rasmi kuitambua serikali ya kundi hilo.

Mbali na suala la kuunda serikali pana na jumuishi na kupambana na ugaidi, kuheshimu haki za binadamu zikiwemo za wanawake ni miongoni mwa masharti yaliyotolewa na nchi mbalimbali na jumuiya za kimataifa kwa ajili ya kuitambua serikali ya Taliban.

Viongozi wa Taliban katika kikao cha Oslo, Norway cha kutafuta uungaji mkono kimataifa

Shirika la habari la Shafaqana la Afghanistan limezinukuu duru za kuaminika ndani ya kundi la Taliban zikieleza kwamba, kimefanyika kikao muhimu cha uongozi wa kundi hilo katika mji wa Kandahar kusini mwa nchi hiyo ambacho kimeajdili suala la kufanya mabadiliko katika baraza la mawaziri  na njia za kuwezesha serikali ya Taliban itambuliwe kimataifa.

Kikao hicho kimeongozwa na kiongozi wa Taliban Haibatullah-Akhundi na kuhudhuriwa na mawaziri wasiopungua 15 wa serikali ya muda ya kundi hilo.

Imeelezwa kuwa kutatua tofauti za ndani ya kundi hilo ni ajenda nyingine iliyojadiliwa katika kikao hicho, japokuwa Taliban yenyewe inakanusha kuwepo kwa tofauti hizo.../

Tags