Mar 24, 2022 13:19 UTC
  • Korea Kaskazini yafanyia majaribio kombora lake kubwa kabisa la balestiki linalovuka mabara

Korea Kusini na Japan zimesema, Korea Kaskazini imefanyia majaribio kile kinachoshukiwa kuwa ni kombora lake kubwa kabisa la balestiki linalovuka mabara.

Taarifa ilyotolewa leo na Makao Makuu ya Vikosi vya Ulinzi Korea Kusini imeeleza kuwa, wamegundua kufyatuliwa "kifaa kirefu kisichojulikana" kutokea Korea Kaskazini. Serikali ya Japan, nayo pia imeripoti urushwaji huo na kusema linaweza likawa ni kombora la balestiki.

Jaribio hilo la leo linaweza likawa la kwanza kuhusisha kombora kubwa zaidi la belistiki la Korea  Kaskazini na kufanyika kwa uwezo kamili tangu mwaka 2017 na linadhihirisha hatua kubwa iliyopigwa na nchi hiyo katika uundaji silaha inayobeba vichwa vya nyuklia vinavyoweza kudondoshwa mahali popote ndani ya Marekani.

Mamlaka za Japan zimesema, jaribio hilo la leo linaonekana ni la "aina mpya" ya Kombora la Belistiki Linalovuka Mabara ICBM ambalo limeruka kwa muda wa dakika 71 katika urefu wa kiliomota 6,000 kwenda juu kutoka usawa wa bahari na masafa yenye umbali wa kilomita 1,100 kutoka eneo lilikorushwa.

Kim Jong-Un

Marekani na Korea Kusini zilitahadhrisha katika wiki za karibuni kwamba huenda Korea Kaskazini inajiandaa kufanya majaribio kamili ya kombora la balestiki linalovuka mabara, ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 2017.

Baada ya kuvunjika mazungumzo ya kuipokonya silaha za nyuklia na makombora Korea Kaskazini, yaliyofanyika baina ya kiongozi wa nchi hiyo Kim Jong-Un na aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump Pyongyang imeamua kuanzisha upya na kwa nguvu kubwa zaidi majaribio yake ya makombora.../

Tags