Mar 25, 2022 02:27 UTC
  • Vita vya Ukraine na mgogoro wa chakula duniani

Zaidi ya nchi 40 zimetia saini barua ya kutaka kuitishwe mkutano wa dharura wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ili kukabiliana na mgogoro wa chakula, ambao huenda ukazidishwa na vita vya Ukraine.

Barua hiyo imesema, takwimu za FAO zinaonyesha kuwa, mgogoro wa Ukraine, mbali na kusababisha kupanda kwa bei ya vyakula duniani, una taathira mbaya katika kilimo, bidhaa ghafi na masoko mengine. Nchi zilizotia saini barua hiyo zimeashiria kuwa, changamoto kubwa za uhaba wa chakula zilikuwepo hata kabla ya kuanza kwa mzozo wa Ukraine na zilishadidi zaidi kutokana na maambukizi ya corona, na kusisitiza kuwa: "Yote haya yanaathiri usalama wa chakula wa mamilioni ya watu katika mataifa kadhaa duniani." 

Wasiwasi kuhusu uhaba wa bidhaa za kimkakati za kilimo duniani umeongezeka zaidi huku vita vya Ukraine vilivyoanza yapata mwezi mmoja uliopita, vikiendelea. Russia na Ukraine ni wazalishaji wakuu wa bidhaa kama vile ngano, shayiri, mahindi, mbegu za mafuta na soya. Uzalishaji wa sekta ya kilimo nchini Ukraine kwa mwaka wa 2022 na miaka miwili ijayo unatabiriwa kuwa mbaya sana kutokana na vikwazo vya Magharibi dhidi ya Russia, vikiwemo vikwazo vya kibiashara na usafirishaji wa baharini, na vilevile na hali ya vita katika maeneo mengi ya Ukrainia. Mshauri wa kiuchumi wa rais wa Ukraine, Oleg Stenko anasema: "Sekta zote za kiuchumi za Ukraine zimeathiriwa na vita, lakini madhara makubwa ya vita yanaonekana zaidi katika sekta ya kilimo." Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) lilisema katika ripoti yake mapema mwezi huu kwamba, asilimia 30 ya mazao ya kilimo ya Ukraine hayawezi kulimwa kutokana na athari mbaya za vita. Vilevile minyororo ya ugavi wa mazao ya kilimo nchini humo inaporomoka.

Russia na Ukraine kwa pamoja hudhamini asilimia 55 ya mauzo ya ngano duniani. Sasa, na baada ya Rusia kuwekewa vikwazo na vita vya Ukraine, usalama wa chakula duniani utavurugika kwa kiasi kikubwa hasa katika nchi zinazoendelea. 

Utegemezi wa dunia kwa akiba ya ngano ya Russia, ambayo inauza nje zaidi ya asilimia 37 ya ngano ya dunia, na Ukraine, ambayo inauza nje zaidi ya asilimia 18 ya ngano ya dunia, na vilevile nafasi ya nchi hizo mbili katika uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa za kimkakati za kilimo duniani, matatizo ya usafirishaji wa shehena na mizigo kutoka bandari za Russia na bandari ya Odessa nchini Ukraine vimeathiri pakubwa misaada ya chakula katika nchi kama vile Yemen, Ethiopia, Afghanistan na Syria. 

Kwa upande mwingine, kutokana na utegemezi mkubwa wa nchi kama Misri, Uturuki, Algeria, Lebanon na Morocco kwa bidhaa za kilimo za Russia na Ukraine, nchi hizi sasa zinakabiliwa na mgogoro usio na kifani. Hivyo tunaweza kusema kuwa, vita vya Ukraine vimezidisha njaa duniani. 

Ni wazi kuwa katika zama hizi za utandawazi na kutegemeana, tukio lolote katika eneo kama vile Ulaya Mashariki huathiri moja kwa moja maeneo mengine ya dunia kama Asia Magharibi na barani Afrika.

Inaonekana kuwa vita vya Ukraine vimekuwa na athari mbaya sana katika nyanja mbalimbali za maisha ya watu katika upeo wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na uchumi, biashara, na usafirishaji wa bidhaa na bidhaa kilimo.

Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) hapo awali ulitahadharisha kuhusu pigo kubwa kwa uchumi wa dunia, hasa kupungua ustawi na kuongezeka mdororo wa kiuchumi duniani. Si hayo tu bali hata suala la kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na ongezeko la joto duniani limeathiriwa na vita vya Ukraine. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema kuwa vita vya Ukraine na athari zake kwenye soko la chakula na nishati vinaweza kuwa na madhara makubwa kwa malengo ya hali ya hewa duniani.

Antonio Guterres

Guterres aliuambia mkutano wa kiuchumi siku ya Jumatatu iliyopita kwamba "Matokeo ya vita vya Russia nchini Ukraine yanahatarisha soko la chakula na nishati duniani na yana madhara makubwa kwa mpango wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa duniani."

Tags