Mar 26, 2022 02:24 UTC
  • Taliban yatangaza mpango wa kuwezesha kufunguliwa tena skuli za wasichana Afghanistan

Msemaji wa wizara ya elimu ya serikali ya Taliban nchini Afghanistan ametangaza kuwa, mpango wa kuwezesha kufunguliwa tena skuli za wasichana kuanzia darasa la saba umekabidhiwa kwa rais wa serikali ya nchi hiyo.

Awali ilikuwa imepangwa kuwa skuli zote za wasichana nchini Afghanistan zitafunguliwa Jumatano ya tarehe 23 Machi baada ya kufungwa kwa muda wa miezi saba, lakini wizara ya elimu ya serikali ya Taliban ilihalifu ahadi yake hiyo iliyokuwa imetoa na kutangaza kuwa, skuli zote za wasichana za kuanzia darasa la saba na kuendelea zitaendelea kufungwa hadi itakapotolewa taarifa nyingine.

Msemaji wa wizara ya elimu ya Taliban, Aziz Ahmad Rayan ametangaza kuwa, mpango wa kuwezesha skuli za wasichana kuanzia darasa la sita na kuendelea kufunguliwa tena, ambao unajumuisha ndani yake utaratibu wa kutenganisha nyakati za usomeshaji na kuweka walimu wanawake wa kuwasomesha watoto wa kike umeshakabidhiwa kwa rais.

Wanafunzi wa kike Afghanistan

Aziz Ahmad Rayan amefafanua kuwa, skuli za wasichana na wavulana inapasa zitenganishwe; na kama kutakuwepo na tatizo la majengo na masuala ya kiuchumi itabidi ratiba ya muda wa masomo ibadilishwe. Aidha ameongeza kuwa, walimu wanawake inawapasa wavae hijabu na wao ndio watapaswa kuwasomesha wanafunzi wa kike.

Uamuzi wa ghafla uliotangazwa na serikali ya Taliban wa kutofunguliwa tena skuli za wasichana nchini Afghanistan katika ngazi ya kati na sekondari, licha ya ahadi iliyotolewa awali ya kufunguliwa, imeamsha hisia kali na kulaaniwa ndani na nje ya nchi hiyo.

Baada ya kushika hatamu za utawala mnamo mwezi Agosti mwaka uliopita, kundi la Taliban lilizifunga skuli za wasichana katika ngazi ya kati na sekondari kwa lengo la kufanya baadhi ya marekebisho.

Jamii ya Kimataifa imekuwa ikisisitiza kuwa, mbali na suala la kuunda serikali pana na jumuishi na kupambana na ugaidi; kuheshimu haki za binadamu zikiwemo za wanawake ikiwa ni pamoja na ya kupatiwa elimu ni miongoni mwa masharti yake ya kuitambua serikali ya Taliban.../

Tags