Mar 26, 2022 13:48 UTC
  • EU: Tuna matumaini mazungumzo ya Vienna yatapelekea kuondolewa vikwazo Iran

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa, Iran na madola makubwa duniani yamekaribia sana kufikia kwenye makubaliano ya kufufua mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Josep Borrel amesema hayo wakati wa kongamano la 20 la Doha na kuongeza kuwa, katika mazungumzo yake ya wakati fulani ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amemwambia kuwa, Umoja wa Ulaya unaunga mkono msimamo wa Tehran wa kupewa dhamana ya kiuchumi na Marekani ya kutojitoa tena kwenye mapatano hayo.

Kabla ya hapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliikuwa amewaambia waandishi wa habari kwamba, Tehran imeieleza wazi Marekani kuwa kamwe haiwezi kuvuka mistari yake myakundu.

 

Hossein Amir-Abdollahian alisema hayo baada ya kuonana na kufanya mazungumzo na Faisal al Miqdad, Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria mjini Damascus na kuongeza kuwa, kama Marekani itaamiliana na mambo katika uhalisia wake, basi Iran nayo itakuwa tayari kufikia makubaliano karibuni tu hivi, kwenye kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa kamati ya pamoja ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Kabla ya hapo pia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alikuwa amesisitizia ulazima wa kuzingatiwa maslahi ya taifa la Iran na mistari myekundu ya Jamhuri ya Kiislamu wakati alipozungumza kwa simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Muhammad bin Abdurahman Aal Thani, na kuongeza kuwa, Tehran iko tayari kikamilifu kufikia makubaliano mazuri, imara na endelevu ya nyuklia.

Tags