Mar 28, 2022 02:27 UTC
  • Kuongezeka mpasuko ndani ya EU kuhusu vikwazo vya mafuta na gesi dhidi ya Russia

Waziri Mkuu wa Poland, Mateusz Morawiecki amedai kuwa, nchi tatu za Ulaya za Ujerumani, Austria na Hungary ni kizuizi katika utekelezaji wa vikwazo vipya dhidi ya Russia na kuzifananisha nchi hizo tatu na breki inayozuia vikwazo vya Magharibi dhidi ya Moscow.

Amedai kuwa, Poland inaunga mkono kikamilifu mpango wa kuwekewa vikwazo vya nishati Russia lakini nchi kama Ujerumani, Austria na Hungary zinazidi kukwamisha jambo hilo na mpaka hivi sasa hazijaacha kununua mafuta na gesi kutoka kwa Russia. Tarehe 20 Machi pia, waziri mkuu huyo wa Poland alitoa pendekezo la kupigwa marufuku kikamilifu biashara baina ya Russia na Umoja wa Ulaya.

Poland ni nchi kubwa zaidi ya Ulaya Mashariki ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Ulaya. Muda wote ina misimamo hasi na ya chuki dhidi ya Russia. Hivi sasa baada ya kutokea vita katika nchi jirani ya Ukraine, imezidi kuwa na uadui na Russia na inaogopa isije nayo ikavamiwa kutokana na misimamo yake hiyo. Si hayo tu, lakini pia Poland pamoja na nchi nyingine za eneo la Baltik yaani Estonia, Latvia na Lithuania muda wote zimekuwa zikichukua misimamo ya kiuadui mno dhidi ya Russia iwe ndani ya Umoja wa Ulaya au ndani ya Jeshi la Nchi za Magharibi NATO na mara wote zimekuwa zikichochea kuwekewa vikwazo Russia. Poland inaongoza nchi za Umoja wa Ulaya ambazo zinataka kushadidishwa vikwazo dhidi ya Russia na inataka vikwazo hivyo vipige marufuku pia kununua mafuta na gesi kutoka Russia.

Jengo likiungua nchini Ukraine katika vita vya nchi hiyo na Russia

 

Hata hivyo msimamo huo wa Poland unapingwa vikali ndani ya Umoja wa Ulaya hususan na nchi kama Hungary. Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orbán, siku ya Ijumaa alimtaka rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, apinge suala la kutumwa silaha zaidi nchini humo na vikwazo vya nishati dhidi ya Russia. Alitoa ufafanuzi kwa kusema kuwa, mambo yanayotakiwa na Zelenskyy yanakwenda kinyume na manufaa ya Hungary na kwamba kuiwekea vikwazo vya nishati Russia kuna maana ya kuporomoka uchumi wa Hungary hata kama vitatekelezwa kwa dakika chache tu. Matamshi hayo ya Waziri Mkuu wa Hungary yanaonesha ni kiasi gani nchi yake inahitajia mno nishati kutoka Russia hasa gesi. 

Hali hiyo ya Hungary inafanana sana na hali ya Ujerumani na Austria. Ujerumani ndiye mnunuaji mkuu wa mafuta na gesi ya Russia. Zaidi ya asilimia 30 ya mafuta ya Ujerumani yanatoka nchini Russia. Aidha kwa uchache asilimia 49 ya gesi inayotumika Ujerumani inatokea Russia. Hali ni hiyo hiyo kwa Austria. Alfred Stern, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mafuta na Gesi la Austria (OMV) ametangaza waziwazi kuwa, asilimia 80 ya gesi inayotumika Austria inanunuliwa kutoka Russia na hivi sasa jambo hilo limekuwa linafanyika kwa karibu miaka 50 kwani gesi ya Russia ndiyo rahisi zaidi kwa Austria. Aidha amesema:  Baadhi yetu (ndani ya Umoja wa Ulaya) hatutaki kujua madhara na hasara kubwa ya kuwekewa vikwazo Russia. Sisi tuko katika mazingira magumu na Ulaya hivi sasa haiwezi kuziba pengo la gesi ya Russia. Ujerumani na Hungary nazo pia zimesema kuwa, haziwezi kuunga mkono vikwazo vya mafuta na gesi dhidi ya Russia kwa sababu si jambo rahisi kwa Ulaya kuweza kuziba pengo hilo.

Nchis za Ulaya ni tegemezi sana nishati ya Russia

 

Tangu vilipoanza vita vya Ukraine, kambi ya Magharibi ikiongozwa na Marekani imeiwekea vikwazo vikali sana vya kiuchumi Moscow, vikwazo ambavyo havijawahi kutokea mfano wake katika historia ya Russia. Vikwazo hivyo vinajumuisha vya kiuchumi, kibiashara, kifedha, kibenki na kuingiza na kutoa bidhaa kutoka Russia. Hata hivyo nchi za Magharibi zimeshindwa kufikiwa mwafaka kuhusu vikwazo vya nishati. Marekani imeiwekea vikwazo vya mafuta na gesi Russia na kuzitaka nchi zote za Ulaya zifanye hivyo, lakini kumezuka mpasuko mkubwa ndani ya Umoja wa Ulaya kuhusu jambo hilo bali mpasuko huo ni mkubwa zaidi ndani ya Umoja wa Ulaya. Kambi ya wafuasi wa Marekani wakiongozwa na Poland wanataka vikwazo vya mafuta na gesi dhidi ya Russia viwekwe haraka, lakini nchi kubwa za Ulaya ambazo zinaangalia mambo katika uhalisia wake kama vile Ujerumani, zinapinga vikali kuifuata kibubusa Marekani katika suala hilo.

Tags