Mar 31, 2022 02:28 UTC
  • Mazungumzo ya Istanbul na sisitizo la uanachama wa Ukraine katika Umoja wa Ulaya

Duru mpya ya mazungumzo kati ya wajumbe wa Russia na Ukraine ilifanyika mjini Istanbul, Uturuki siku ya Jumanne iliyopita. Baada ya mazungumzo na Russia, mkuu wa ujumbe wa Ukraine, David Arakhamia, alisema kuwa hakuna mtu anayeweza kuizuia Ukraine kujiunga na Umoja wa Ulaya.

Alisema kuwa pande hizo mbili bado hazijafikia makubaliano kuhusu baadhi ya masuala, na kwamba upande wa Ukraine haujapata kibali chochote kutoka kwa Russia. Ameongeza kuwa iwapo kutapatikana makubaliano na Russia, Ukraine itaitisha kura ya maoni.

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy pia alisema Jumanne usiku kwamba kuna ujumbe chanya katika mazungumzo ya amani na Russia. Hata hivyo amesisitiza kuwa vikwazo dhidi ya Russia havitakiwi kuondolewa hadi vita vitakapokomeshwa.

Kwa upande wake, Moscow imetangaza kuwa inakusudia kupunguza kwa kiasi kikubwa uwepo wake wa kijeshi Kaskazini mwa Ukraine kufuatia mazungumzo kati ya wajumbe wa nchi hizo mbili mjini Istanbul. Hata hivyo Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, imekanusha madai hayo, ikisema haijaona dalili yoyote ya kurudi nyuma majeshi ya Russia. 

Suala muhimu lililopewa mazingatio zaidi katika mazungumzo ya Istanbul ni hatua ya Ukraine ya kukubali kwamba haitoegemea upande wowote wala kuwa mwanachama katika Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO). Wakati huo huo imesisitiza haja ya kuwa mwanachama katika Umoja wa Ulaya, suala ambalo limekubaliwa na Russia. Hapo awali, Zelenskyy alitupilia mbali msimamo wake wa kabla akitangaza kuwa yuko tayari kuachana na matakwa yake katika mchakato wa amani na Moscow na kuwa taifa lisiloegemea upande wowote katika makabiliano kati ya Magharibi na Russia.

Mazungumzo baina ya Russia na Ukraine

Kufuatia matukio ya 2014 na kuanzishwa serikali inayounga mkono Magharibi nchini Ukraine, suala la uanachama wa nchi hiyo katika Umoja wa Ulaya na shirika la NATO lilijumuishwa katika marekebisho ya Katiba ya Ukraine ili kuunganishwa na kambi ya Magharibi. Marekani na washirika wake wa Ulaya pia waliunga mkono uanachama wa Ukraine katika shirika la kijeshi la NATO, lakini hawakuwa na maoni chanya kuhusu suala la uanachama wa nchi hiyo katika Umoja wa Ulaya. Baada tu ya mashambulizi ya Russia dhidi ya Ukraine, Rais wa nchi hiyo, Volodymyr Zelenskyy alitaka Ukraine ikubaliwe kama mwanachama wa Umoja wa Ulaya akisisitiza kuwa, watu wa Ukraine wana haki ya kujiunga na umoja huo na kwamba kukubaliwa uanachama huo kutaonyesha uungaji mkono wa mataifa ya Ulaya kwa Kyiv. Petro Poroshenko, rais wa zamani wa Ukraine anasema: "Kujiunga Ukraine katika Umoja wa Ulaya na NATO ni lengo la kimkakati kwa taifa hili." Hata hivyo, Umoja wa Ulaya haukutoa jibu mwafaka kwa ombi la Zelenskyy. Tunaweza kusema kuwa, jibu la Brussels kwa ombi la Kyiv limekuwa baridi na hasi. Upinzani mkubwa wa Ujerumani, nchi kubwa na yenye uchumi mkubwa zaidi katika Umoja wa Ulaya, dhidi ya Ukraine kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya umekatiza matumaini ya Rais wa Ukraine ya kupata uanachama haraka katika umoja huo. Ingawa Bunge la Ulaya limeidhinisha ombi la Ukraine la kupewa uanachama katika umoja huo, lakini Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen alisema suala hilo ni mchakato unaochukua muda mrefu. Amesema kuwa watu wa Ukraine ni wa familia ya Ulaya, lakini uanachama katika umoja huo una mchakato ambao lazima ufuatwe.

Kwa kuzingatia viwango na vigezo vya EU, na jinsi Kyiv ilivyombali na viwango hivyo hasa katika suala la kupambana na ufisadi wa kifedha na wa kiutawala, kimsingi haiwezekani kukubaliwa ombi la Zelinskyy la Ukraine kujiunga na EU katika kipindi kifupi. Kwa sasa Ukraine inashika nafasi ya 117 katika masuala ya kupambana na ufisadi na rushwa duniani na ni miongoni mwa nchi zinazoongoza barani Ulaya katika ufisadi wa kifedha na kiutawala.

Hali ya kiuchumi ya Ukraine pia imekuwa ikizorota katika miaka ya hivi karibuni. Haya yote yanapunguza uwezekano wa Ukraine kujiunga na Umoja wa Ulaya. Hii ni pamoja na kuwa, moja ya masharti muhimu zaidi yaliyoainishwa na Umoja wa Ulaya kwa nchi zinazotafuta uanachama katika umoja huo ni kutatua migogoro yote ya mipaka na majirani zao.

Hivyo, licha ya kwamba Russia haipingi suala la Ukraine kupewa uanachama katika Umoja wa Ulaya, lakini Moscow inafahamu vyema kwamba mchakato huo ni mrefu sana na hivyo haijaonesha unyeti wowote katika suala hili. Kilicho muhimu kwa Russia, ambacho pia kimetimizwa, ni Ukraine kutokuwa mwanachama katika Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO).

Tags