Apr 03, 2022 03:32 UTC
  • WFP yatahadharisha kuhusu uhaba wa chakula duniani

Wakati vita vya Russia na Ukraine vikiendelea, upatikanaji wa chakula umekuwa mgumu zaidi kwa watu wengi duniani, huku msemaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) akisema vita vya Russia na Ukraine vimezidisha dola milioni 71 kwa mwezi kwenye gharama zinazotumiwa na shirika hilo la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kununua chakula.

Ripoti zinasema kanda za Asia Magharibi na Afrika Kaskazini zimo katika hatari ya kukumbwa na mzozo wa chakula kutokana na vita vya Russia na Ukraine. Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) linakadiria kuwa watu milioni 13 duniani kote huenda wakakabiliwa na uhaba wa chakula kutokana na vita vya Russia na Ukraine.

Ukraine na Russia ndio wazalishaji wakuu wa bidhaa za kilimo, kwa kadiri kwamba takriban asilimia 30 ya ngano inayouzwa nje ya nchi, asilimia 20 ya mauzo ya mahindi na asilimia 75 ya mafuta ya alizeti duniani yanadhaminiwa kutoka eneo la Bahari Nyeusi. Hivyo vita vya sasa kaika eneo hilo vimezusha wasiwasi wa kusababisha uhaba wa chakula.

Mkurugenzi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Martin Frick, anasema: "Hii ni vita ambayo dunia haiwezi kuvistahamili na vitaifanya itakabiliwe na tatizo la chakula. Nchi yenye watu milioni 40, ambayo ilikuwa ikizalisha chakula kikuu kwa watu milioni 400 duniani, sasa inahitaji msaada wa chakula. Na ikiwa Ukraine haitalima ngano katika siku zijazo, ulimwengu utakabiliwa na shida ya chakula."

Athari mbaya za mgogoro huo zitahisika zaidi kwa nchi maskini, hasa nchi za Afrika, kutokana na kupanda kwa gharama za chakula, mafuta na usafiri, kwa sababu chakula na nishati ni bidhaa mbili muhimu kwa watumiaji. 

Ripoti zinaonesha kuwa, nchi 35 za Afrika zinategemea uagizaji wa chakula kutoka eneo la Bahari Nyeusi, na Rusia na Ukraine zina jukumu kubwa katika kukidhi mahitaji ya ncho hizo; hivyo hali hii itaathiri sana usalama wa chakula wa nchi hizo. Katika mkondo huo, Mkuu wa Benki ya Maendeleo Afrika, Akinwumi Adesina, amesema kuwa, theluthi moja ya nafaka zinazotumiwa Afrika Mashariki inatoka katika nchi mbili hizo; huku Misri ikiwa imeathirika pakubwa. Hali kama hii inashuhudiwa pia huko Algeria, Morocco na Somalia na katika nchi nyingine kadhaa. Amesema iwapo hali hii haitadhibitiwa haraka iwezekanavyo, bara la Afrika litayumba. Vita vya Russia na Ukraine pia vimeathiri pakubwa misaada ya chakula katika nchi zlizoathiriwa na vita kama vile Yemen, Ethiopia, Afghanistan na Syria. 

Akizungumzia hali ya Yemen Mkurugenzi Mtendaji wa Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa, David Beasley amesema mgao wa chakula wa watu milioni nane nchini humo umepunguzwa kwa asilimia 50. 

Nchi za Magharibi zimekua na nafasi kubwa zaidi katika kuibua mgogoro huu kwa kuweka vikwazo vizito, kuchochea vita na kuiunga mkono Ukraine kwa kuipatia kila aina ya silaha. Mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa, Vasily Nebenzia, amesema kuwa sababu halisi za mgogoro mkubwa wa chakula duniani si hatua za Russia, bali wendawazimu wa vikwazo vya Magharibi dhidi ya Russia.

Vasily Nebenzia

Sababu nyingine ya mgogoro huo ni sera ya nchi za Magharibi ya kujilimbikizia bidhaa muhimu kama chakuka katika kipindi hiki, kwa kadiri kwamba, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO), Ngozi Okonjo-Iweala amezionya nchi zinazozalisha chakula kuhusu tabia ya kujilimbikizia bidhaa na akasema kwamba, ni muhimu sana kujiepusha na hali iliyojitokeza wakati wa kilele cha janga la Covid-19. Bi Okonjo-Iweala alikuwa akiashiria hatua ya nchi za Magharibi ya kujilimbikizia chanjo za corona wakati maelfu ya watu walipokuwa wakiaga dunia kutokana na kutopata chanjo ya virusi vya corona katika maeneo mbalimbali ya dunia hususan katika nchi zinazoendelea. 

Kwa sasa, bei ya vyakula kama vile ngano na nafaka imefikia kiwango cha juu zaidi, na inaonekana kuwa iwapo mwenendo huu utaendelea hali itazidi kuwa ngumu zaidi kwa nchi zote, haswa zile dhaifu kiuchumi. 

Tags