Apr 07, 2022 01:56 UTC
  • Vladimir Putin
    Vladimir Putin

Katika hotuba aliyotoa siku ya Jumanne, Rais Vladimir Putin wa Russia amelaani mashinikizo yanayotolewa na nchi za Ulaya dhidi ya shirika la Gazprom, ambalo husafirisha gesi ya nchi hiyo kwenda Ulaya, na kutishia kuchukua hatua za kulipiza kisasi.

Putin pia ametoa wito wa kuchukuliwa "tahadhari zaidi" katika uuzaji nje bidhaa za chakula akisema Russia itatazama upya siasa za mauzo yake ya kilimo kwa nchi zisizo rafiki. Akizungumza karibuni katika kikao cha kujadili kilimo na bidhaa za chakula, Rais Putin amesema: "Russia itakabiliana na suala la mauzo ya chakula nje ya nchi kutokana na uhaba uliopo kimataifa." Amesema: “Mwaka huu, kutokana na uhaba wa chakula duniani, ni lazima tuwe makini zaidi katika kuuza chakula chetu nje ya nchi, yaani, tufuatilie kwa makini vigezo vya mauzo hayo kwa nchi ambazo zinatuchukia hadharani."

Putin amesisitiza haja ya kuangaliwa upya sera ya Russia kuhusu mauzo ya chakula na mazao ya kilimo nje ya nchi kwa kuzingatia kuendelea vita vya Ukraine na athari zake mbaya kwa mauzo ya nje ya ngano, shayiri na mahindi, pamoja na mafuta ya alizeti ya wazalishaji wakuu wawili hao wa bidhaa hizo.

Ukraine imeingia katika vita vikubwa ambavyo matokeo yake hasi sasa yanaonekana wazi katika sekta ya kilimo, ambapo mazao ya kilimo yamepungua sana mwaka huu na yanatazamiwa kuendelea kupungua miaka miwili ijayo. Hali hiyo imepelekea mazao ya kilimo ya Ukraine kupungua kwa nusu na utabiri unaonyesha kwamba sehemu kubwa ya ardhi ya kilimo ya nchi hiyo haitatumika kwa shughuli hiyo mwaka ujao. Makumi ya meli zilizokuwa zimebeba bidhaa za chakula kutoka Ukraine zimekamatwa na Russia katika Bahari Nyeusi, hivyo hazitaweza kufikisha bidhaa hizo katika masoko yaliyokusudiwa, kwa uchache hadi pale suala la vita vya Ukraine litakapotatuliwa.

Manowari za Russia zikiwa katika Bahari Nyeusi

Russia, kwa upande mwingine, ikiwa moja ya wauzaji wakubwa wa ngano ulimwenguni, ambapo wateja wao wako Asia Magharibi na Afrika, kutokana na kupanda kwa kasi kwa bei ya bidhaa hii na mazao mengine ya kimkakati ya kilimo kama vile shayiri, mahindi na mbegu za mafuta, inakusudia kutumia bidhaa hizo kama chombo cha kutoa mashinikizo dhidi ya nchi zisizo rafiki. Nchi hizo ni pamoja na Albania, Andorra, Australia, Uingereza, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, Iceland, Canada, Liechtenstein, Micronesia, Monaco, New Zealand, Norway, Korea Kusini, San Marino, Northern Macedonia, Singapore, Marekani, Taiwan, Ukraine, Montenegro, Uswizi na Japan.

Kutokana na ukubwa wa ardhi yake yenye rutuba na hali nzuri ya hewa, Russia ndio mzalishaji mkubwa zaidi wa ngano ulimwenguni na kati ya mwaka 2020 na 2021 ilifanikiwa kuchukua nafasi ya kwanza duniani kwa kuzalisha zaidi ya tani milioni 37 za ngano. Ukraine nayo ilichukua nafasi ya tano duniani katika kipindi hicho hicho kwa kuzalisha zaidi ya tani milioni 18 za ngano. Kuondolewa Ukraine katika soko la kimataifa la bidhaa za kimkakati za kilimo na uamuzi wa Russia wa kutazama upya sera zake kuhusu mauzo ya ngano kwa nchi zisizo rafiki bila shaka ni mambo yatakayoongeza bei ya ngano, ambayo ni bidhaa ya kimkakati kimataifa.

Hali hii itakuwa na matokeo mengi mabaya kwa nchi ambazo zimekuwa waagizaji wakuu wa bidhaa za chakula kutoka Russia na Ukraine. Wakati huo huo, kupunguzwa kwa mauzo ya ngano kutoka Russia na kuondolewa Ukraine katika soko la wauzaji wakuu wa ngano duniani kutazipelekea nchi nyingine, ambazo ni wauzaji wakuu wa bidhaa hiyo ya kimkakati, kuwa waangalifu katika mauzo yao ya nje na kuzingatia maslahi ya raia wao kwanza kabla ya kufikiria maslahi ya mataifa mengine. Kufutia Russia kutangaza marekebisho ya sera za mauzo ya bidhaa zake za kilimo kwa nchi zisizo rafiki, Putin ameibua hali mpya katika soko la kimataifa la bidhaa za kimkakati za chakula na kuanzisha milingano na vigezo vipya katika soko hilo.

Kilimo cha ngano

Umoja wa Mataifa una wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya chakula duniani baada ya vita vya Ukraine na athari zake mbaya katika uzalishaji na uuzaji nje wa bidhaa za kimkakati za kilimo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne kwamba uvamizi wa Russia dhidi ya Ukraine ni mojawapo ya changamoto kubwa zaidi kwa mfumo wa kimataifa kutokana na utambulisho, ukali na matokeo yake. Amesema: "Vita hivyo vinatoa shinikizo zaidi kwa nchi zinazoendelea, na kuziweka nchi 74 zenye watu zaidi ya bilioni 1.2 katika hatari ya kupanda kwa gharama za chakula, nishati na mbolea. Sasa tunashuhudia baadhi ya nchi zilizokuwa katika mazingira magumu zikitumbukia kwenye mgogoro na kudhihiri dalili za machafuko makubwa ya kijamii."

Tags