Apr 10, 2022 04:15 UTC
  • China: Marekani inatesa wafungwa kwenye jela za siri, haina haki ya kuzinyooshea kidole nchi nyingine

China imeituhumu Marekani kuwa inafanya mateso ya kutisha dhidi ya wafungwa katika jela za siri (black sites) katika nchi washirika, ikisisitiza kwamba Washington haina haki ya kuikosoa nchi nyingine yoyote kwa ukiukaji wa haki za binadamu.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Zhao Lijian amesema, shirika la ujasusi la Marekani CIA limeanzisha vituo vyeusi (jela za siri) katika nchi nyingi kwa kisingizio cha "vita dhidi ya Ugaidi" inakowashikilia kwa siri watu wanaotuhumiwa kuwa ni magaidi na kuwalazimisha kukiri makosa kupitia njia ya mateso.

Zhao ameongeza kuwa: "Hata hivyo, hadi sasa hakuna afisa hata mmoja wa Marekani aliyekamatwa na kuwajibishwa kwa kubuni, kuidhinisha au kutekeleza mpango wa kuwaweka kuweka kizuizini kwa siri na kuwatesa watuhumiwa."

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema, ukweli huzungumza zaidi kuliko maneno, na kusisitiza kuwa jela hizo za siri za Marekani katika pembe mbalimbali za dunia zinaonesha wazi kwamba, Washington haina haki ya kuzinyooshea kidole nchi nyingine kwa jina la demokrasia na haki za binadamu.

 Zhao Lijian

Zhao Lijian amesema, Marekani inapaswa kukomesha mara jela hizo za siri duniani kote, kutafakari kwa dhati uhalifu wake, kuomba msamaha, kuwalipa fidia wahanga wa uhalifu huo, na kuwawajibisha wale wote walioidhinisha na kutekeleza mateso.

Matamshi hayo ya Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya China yametolewa baada ya gazeti la Guardian la Uingereza kuchapisha ripoti mpya ya iliyofichua mwezi uliopita kwamba mfungwa katika kituo cha siri cha CIA nchini Afghanistan alitumika kama kielelezo hai (panya wa maabara) cha kuwafunza wachunguzi ambao walijipanga kwa zamu wakigonga kichwa cha raia huyo wa Afghanistan kwenye ukuta, na kumwacha akiwa na uharibifu wa ubongo.

Tags