Apr 11, 2022 05:02 UTC
  • Umoja wa Ulaya wachochea vita Ukraine: Mchezo wa Brussels kwenye uwanja wa Washington

Huku akisema kuwa mvutano kati ya Ukraine na Russia utamalizikia tu katika medani ya vita, Joseph Borrell, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya ametoa wito wa kutatuliwa kijeshi mzozo uliopo kati ya pande hizo.

"Vita vya sasa vitaishia tu kwenye uwanja wa vita. Tumetoa nyongeza ya Euro milioni 500 msaada wa EU kwa Ukraine, na utumaji silaha utaendana na mahitaji ya Ukraine," Borrell ameandika katika ujumbe wake wa Twitter. Borrell pia ametoa wito wa kuongezwa vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Russia na hasa katika sekta ya nishati.

Msimamo wa kivita wa sasa wa Umoja wa Ulaya kuhusu mzozo wa kijeshi nchini Ukraine unakinzana na msimamo rasmi wa Brussels unaoonekana kuwa wa amani kuhusu mizozo ya kikanda na kimataifa. Umoja wa Ulaya, kwa uchache hadi sasa, umekuwa ukijidhihirisha kuwa mpenda amani na hivyo kufuatilia harakati za amani kwa ajili ya kutatua migogoro ya kikanda na kimataifa. Daima umekuwa ukisisitiza haja ya kutatuliwa kwa amani migogoro ya kimataifa kupitia mazungumzo na ufumbuzi wa kisiasa. Hata hivyo, Borrell sasa ametoa wito wa wazi wa kuendelea vita vya Ukraine kati ya jeshi na wanamgambo wanaoiunga mkono Russia kwa upande mmoja na jeshi na wanamgambo wanaoiunga mkono Ukraine kwa upande wa pili.

Marekani yatumia Ukraine kuishinikiza Russia

Hili linaeleweka kwa kuzingatia kuongezeka ushirikiano kati ya pande mbili za Bajari ya Atlantiki tangu Rais wa chama cha Demokrasia Joe Biden aingie madarakani nchini Marekani mnamo Januari 2021. Biden, tofauti na alivyokuwa mtangulizi wake, Donald Trump, ambaye alichukua mtazamo wa upande mmoja na hivyo kuvuruga uhusiano wa pande mbili za Bahari ya Atlantiki katika nyanja mbalimbali za kisiasa, kibiashara, kijeshi na kiusalama, amekuwa akifanya juhudi kubwa za kuimarisha uhusiano na nchi za Ulaya. Amekuwa akitafuta uungaji mkono wa Ulaya katika kukabiliana na maadui na wapinzani wa Washington.

Dhihirisho la ushirikiano huo linaweza kuonekana wazi katika msimamo mmoja thabiti kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya kuhusiana na  Russia na shinikizo linaloongezeka kila siku dhidi ya Moscow kwa kisingizio cha vita vya Ukraine. Operesheni ya kijeshi ya Russia nchini Ukraine sasa inaipa Marekani na washirika wake fursa muhimu ya kuingia katika awamu ya vita vya niaba na Russia kwa kutoa msaada mkubwa wa kijeshi na kijasusi kwa Kyiv. Kwa muda mrefu sasa Marekani imekuwa ikitoa wito wa kusambaratishwa Russia na hata kugawanywa nchi hiyo katika majimbo tofauti yanayojitawala. Wasiwasi mkubwa wa Washington na Brussels kuhusu kuwekwa tena  makombora ya nyuklia ya Russia karibu na mipaka ya magharibi mwa Ulaya, na hatua za Putin za kukabiliana na siasa na vitendo vya Magharibi ni mambo ambayo yamezipa pande mbili hizo fursa ya kipekee ya kupunguza nguvu za Russia. Hii ni katika hali ambayo uhusiano wa Umoja wa Ulaya na Russia unatofautiana kimsingi na uhusiano wa Marekani na Russia, na bila shaka hatua ya Ulaya kuamua kucheza kwenye uwanja wa Marekani itakuwa na madhara makubwa kwa umoja huo.

Umoja wa Ulaya unatumiwa vibaya na Marekani katika mgogoro wa Ukraine

Kuhusu suala hilo, katika hali ambayo maslahi ya Ulaya yanailazimu kuendelea kuagiza nishati kutoka Russia kutokana na utegemezi wake wa asilimia 40 kwa gesi na asilimia 25 kwa mafuta ya Russia, mkuu wa sera za kigeni wa EU anataka kuzidishwa vikwazo vya Ulaya dhidi ya Russia na kusimamishwa uagizaji wa nishati kutoka nchi hiyo. Borrell alitangaza Alhamisi kwamba vikwazo vya mafuta dhidi ya Russia vitakuwa kwenye ajenda ya mkutano wa Baraza la Mambo ya Kigeni la EU mnamo Aprili 11. Msimamo huo unaendana kikamilifu na hatua za Washington katika uwanja huo. Siku ya Ijumaa, Rais Joe Biden alitia saini kuwa sheria mswada uliopitishwa na Bunge la Congress kuhusu kusitishwa uhusiano wa kibiashara na kupiga marufuku uagizaji wa nishati kutoka Russia.

Bila shaka, msimamo huo mkali wa Joseph Borrell umekabiliwa na majibu makali kutoka Moscow. Maafisa wa Russia wanafahamu vyema kwamba matamshi hayo kwa hakika ni ishara ya kuendelea hatua za pamoja za Brussels na Washington kwa lengo la kuzidisha mashinikizo dhidi ya Moscow. Akilaani matamshi ya Josep Borrell kuhusu mzozo wa Ukraine, Vyacheslav Volodin, Spika wa Duma ya Russia, alisema kuwa yeyote anayetaka mgogoro na ghasia ziendelee anapaswa kufutwa kazi mara moja. Amesema: NATO, pamoja na Washington, hazitaki Ukraine iwe nchi huru, isiyoegemea kambi fulani."

Tags