Apr 12, 2022 11:04 UTC
  • Duru ya pili ya uchaguzi Ufaransa; mchuano baina ya Macron na Le Pen

Uchaguzi wa Rais nchini Ufaransa umemalizika huku Emmanuel Macron na Marine Le Pen wakiingia katika duru ya pili. Kwa utaratibu huo, siku 14 zijazo yaani tarehe 24 mwezi huu hatima ya uchaguzi huo itajulikana na mshindi wa duru hiyo atapata tiketi ya kuingia katika ikulu ya Elizeh.

Matokeo ya awali ya uchaguzi huo yanaonyesha kuwa, Macron amepata asilimia 28.5 ya kuwa na Le Pen asilimia 24.4 na hivyo kuingia katika duru ya pili ya uchaguzi. Wagombea 12 kutoka vyama mbalimbali wameshiriki katika duru hiyo ya uchaguzi wa rais wa Ufaransa huku washindani wakuu wakiwa ni Macron na Le Pen. Wanasiasa hao wawili sasa wameingia katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais iliyopangwa kufanyika tarehe 24 ya mwezi huu wa Aprili; na ni wazi kuwa siku zijazo zitakuwa siku muhimu za maamuzi kwa mustakabali wa kisiasa na kiuchumi wa Ufaransa na Umoja wa Ulaya.   

Emmanuel Macron kuchuana na Marine Le Pen katika duru ya pili ya uchaguzi

Jambo la kutilia maanani katika uchaguzi huo wa rais wa Ufaransa ni ushiriki wa kiwango cha chini wa wananchi; suala ambalo limeibua wasiwasi wa kijamii nchini humo. Takwimu zinaonyesha kuwa, ushiriki wa wapiga kura katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais wa Ufaransa kama ilivyotarajiwa umepungua kwa kiasi kikubwa. Takwimu zilizotolewa na wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa zinaonyesha kuwa, kiwango cha ushiriki wa wananchi katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais wa mwaka huu kilikuwa asilimia 25.48; kiasi ambacho kimetajwa kuwa ni kikubwa cha kupungua kwa ushiriki wa wananchi kulinganisha na duru iliyopita. 

Pamoja na hayo, ni dhahir shahir kuwa marhala kuu ya mchuano wa kiti cha rais Ufaransa imeanza kwa kutangazwa matokeo hayo ya duru ya kwanza ya uchaguzi. Macron ambaye ni rais kijana zaidi kuwahi kuongoza katika historia ya Ufaransa katika miaka mitano ya uongozi wake amekumbwa na migogoro mingi yakiwemo maandamano ya "Harakati ya Vizibao vya Njano" na maambukizi ya UVIKO-19. Emmanuel Macron ambaye mwaka 2017 aligusia juu ya kuboreka hali ya uchumi wa Ufaransa hivi sasa ameingia katika mchuano wa kuwania kiti cha rais kwa mara nyingine tena huku mfumuko wa bei ukivunja rekodi nchini humo na katika Umoja wa Ulaya ambapo gharama za makazi  zimeongezeka pakubwa kuliko wakati wa janga la Corona. Pamoja na kuwa akthari ya wananchi wa Ufaransa wanalalamikia utendaji wa Macron lakini misimamo yake ndani ya Umoja wa Ulaya na sasa kuhusu mgogoro wa Ukraine imewafanya wengi kumchukulia kuwa ndiye atakayeibuka na ushindi katika uchaguzi huo.  

Harakati ya vizibao vya njano nchini Ufaransa 

Emiliano Alessandri mwanachama wa Taasisi ya German Marshall Fund anaamini kuwa, ni vigumu kulinganisha misimamo ya Emmanuel Macron na viongozi wengine kuhusu mgogoro wa Ukraine. Vilipokaribia vita vya Ukraine, Macron alifanya safari mjini Moscow; ziara iliyoibua makelele mengi; na tokea hapo Ufaransa imejidhihirisha kuwa mstari wa mbele miongoni mwa pande tatu kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na uwezo wa kujilinda muungano wa Nato; na wakati huo huo ikiiunga mkono Ukraine sambamba na kuendeleza uhusiano wake na Vladimir Putin licha ya Russia kutengwa pakubwa kimataifa."  

Emanuel Macron ameweka wazi kuhusu sera zake kuu za kigeni, na kubainisha kuwa juhudi zinapasa kufanywa ili kuwa na Ulaya iliyo huru zaidi na kuwa na Umoja wa Ulaya wenye rasilimali kama wenzo bora zaidi wa kutetea maslahi ya Ufaransa duniani. Hata hivyo katika upande mwingine, Bi Marine Le Pen amedhihirisha mitazamo yake ya utaifa katika mchuano huo wa kuwania kiti cha urais nchini Ufaransa. Mgombea huyo ametaka Ufaransa ijitoe ndani ya muungano wa Nato huku akihoji juu ya mikataba ya Umoja wa Ulaya katika kile alichokitaja kuwa ili kuwa huru Ufaransa. Si hayo tu, bali Le Pen ameahidi kuwa, iwapo atashinda kiti cha urais atadhibiti pia wahajiri na kuboresha uchumi wa nchi hiyo. Pamoja na ahadi zake hizo, chunguzi za maoni zinaonyesha kuwa, Macron ataibuka na ushindi katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais wa Ufaransa.

Ala kulli hal, inaonekana kuwa siku 14 zijazo zitakuwa siku muhimu sana katika uga wa siasa za Ufaransa na Ulaya. Hii ni kwa sababu, wananchi wa Ufaransa na Ulaya watashuhudia mabadiliko makubwa iwapo Le Pen ataibuka na ushindi katika uchaguzi huo wa rais; mabadiliko ambayo si tu kuwa yataathiri siasa za utaifa za Ufaransa bali yatabadili pia taswira ya kisiasa ndani ya Umoja wa Ulaya. 

Tags