Apr 14, 2022 02:24 UTC
  • Le Pen awaahidi wapiga kura kupiga marufuku hijabu na kuchinja wanyama Kiislamu Ufaransa

Mgombea urais wa Ufaransa kwa tikiti ya chama chenye siasa kali cha mrengo wa kuli, Marine Le Pen, amesema iwapo atashinda kiti cha urais, atapiga marufuku kuchinja wanyama kwa njia ya Kiislamu ya Kiyahudi, na vilevile vazi la staha la mwanamke wa Kiislamu, hijabu.

Le Pen amedai kuwa atafanya hivyo ili kujibu matakwa ya Wafaransa waliowengi. Hata hivyo duru mbalimbali za habari zinasema, uamuzi huo unatokana na sera na mitazamo ya chuki na ubaguzi ya mwanasiasa huyo wa Ufarana dhidi ya Uislamu na wahajiri. 

Kwa upande mwingine, mgombea huyo mwenye siasa kali za mrengo wa kulia wa Ufaransa amekariri azma yake ya kupiga vita kile alichokitaja kama "aidiolojia na itikadi ya Kiislamu", na kupiga marufuku vazi la hijabu.

Amewaambia wapiga kura wa Ufaransa kwamba: "Hatupaswi kuacha nafasi yoyote kwa aidiolojia ya Kiislamu, au kukabiliana nayo kwa upole; kwa hiyo tumetayarisha muswada wenye lengo la kupiga marufuku jambo hili katika ardhi ya Ufaransa, na kupiga marufuku ufadhili na taasisi zinazoeneza itikadi za Kiislamu, na maeneo ambako itikadi hizi zinafunzwa."

Le Pen amesema analitambua vazi la hijabu ya Kiislamu kuwa nembo ya aidiolojia ya Kiislamu, na kwamba 'anatumai kuwaokoa wanawake wote na vazi hulo.'

Rais anayemaliza muda wake wa Ufaransa, Emmanuel Macron alipata asilimia 28.1 ya kura za duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais akifuatiwa kwa karibu na mgombea wa chama cha mrengo wa kulia cha National Rally, Marine Le Pen aliyepata asilimia 23.3. Wagombea hao wawili sasa watachuana katika uchaguzi wa duru ya pili uliopangwa kufanyika tarehe 24 Aprili. 

Tags