Apr 14, 2022 02:25 UTC
  • Kiwango cha maambukizi ya corona chapungua duniani kwa wiki ya tatu mtawalia

Kiwango cha maambukizi ya Covid-19 duniani kimepungua kwa kwa wiki ya tatu mfululizo hadi kufikia tarehe 10 Aprili.

Shirika la habari la Iran, IRNA limeripoti kuwa, takwimu mpya katika maeneo sita yanayosimamiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha mwelekeo wa kupungua idadi ya kesi za maambukizi na vifo vinavyosababishwa na virusi vya corona.

Kufikia Aprili 10, kulikuwa na kesi zaidi ya milioni 496 zilizothibitishwa za maambukizi ya Covid-19 na zaidi ya vifo milioni 6 kote duniani.

Virusi vya corona vimekuwa na mabadiliko manne hatari ya kijeni na spishi za Alpha, Beta, Delta, Gamma, na aina ya Omicron ndio inayoisumbua dunia katika miezi ya hivi karibuni. 

Wakati huo huo Japan imetangaza kesi yake ya kwanza ya aina mpya ya COVID-19 ijulikanayo kama Omicron XE ambayo imegunduliwa kwa mara ya kwanza nchini Uingereza.

Hadi kufikia  Aprili 5, kesi 1,125 za Omicron XE zilikuwa zimegunduliwa nchini Uingereza wakati ambao idadi hiyo ilikuwa ni 637 hadi kufikia Machi 25.

Wataalamu wanasema ni mapema kubaini makali ya aina hii mpya ya COVID-19 au uwezo wake wa kutoathiriwa na chanjo zilizopo.

Tags