Apr 15, 2022 05:20 UTC
  • Putin asisitiza udharura wa kuendelea operesheni za kijeshi za Russia nchini Ukraine

Akizungumza Jumanne katika kikao cha wafanyikazi wa kituo cha anga cha Vostochny Mashariki ya Mbali nchini Russia, kuhusu kufikiwa malengo ya shambulio la Ukraine, ambayo aliyataja kuwa ya "wazi kabisa na bora," Rais Vladimir Putin amesema: Hakuna shaka hali itaendelea kuwa hivyo."

Rais Putin amesisitiza: "Lengo kuu (la operesheni ya kijeshi ya Russia nchini Ukraine) ni kuwasaidia watu wa Donbass, ambao tumetambua uhuru wao.  Kutokana na shinikizo ya Wamagharibi, maafisa wa Kyiv walikataa kufuata makubaliano ya Minsk yenye lengo la kusuluhisha kwa amani mzozo wa Donbass." Kwa mujibu wa Putin, magenge ya wanazi mamboleo yalikuwa yanaeneza harakati zao huko Kyiv, na bila shaka yangeibua mzozo na Moscow, suala pekee likiwa hilo lingetokea lini.

Kwa hakika, Rais wa Russia anaamini kwamba vita vya Ukraine havingeweza kuepukika. Sababu ya hilo, kwa maoni yake, ni kukataa serikali ya Kyiv kutekeleza makubaliano ya Minsk ili kufikia usitishaji vita mashariki mwa Ukraine na utekelezaji wa ahadi zake kwa eneo hilo, kuenea mafashisti na manazi mamboleo na mashambulizi ya jeshi la Ukraine na wanamgambo wa nchi hiyo dhidi ya Donbass.

Wakati huo huo, Putin anasisitiza kwamba vita kati ya Russia na Ukraine havingeepukika, kutokana na mazingira na mwenendo wa matukio ya kieneo. Suala hilo lilionekana kutoepukika kutokana na Ukraine kuomba mara kwa mara kujiunga na shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO na wakati huo huo kupokea msaada mkubwa wa kijeshi kutoka shirika hilo na Marekani. Mambo yariharibika zaidi hasa baada ya NATO kusisitiza kujitanua kuelekea mashariki kufuatia hatua za hivi karibuni za shirika hilo karibu na mpaka wa Russia.

Silaha za Marekani kwa Ukraine

Tarehe 21 Februari, Rais Vladimir Putin kwa mara ya kwanza alizikosoa nchi za Magharibi kwa kutozingatia masuala ya usalama ya Moscow, na kutangaza kuwa nchi yake ilikuwa imetambua uhuru wa Jamhuri za Watu wa Donetsk na Luhansk, na kutia saini makubaliano ya ushirikiano na urafiki na viongozi wazo katika Ikulu ya Kremlin. Baadaye, Februari 24, Putin aliamuru operesheni maalumu ya kijeshi katika eneo la Donbass kujibu ombi la usaidizi wa kijeshi kutoka kwa viongozi wa Donetsk na Luhansk.

Matamshi ya Putin yameungwa mkono na Rais Alexander Lukashenko wa Belarus, ambaye anahesabiwa kuwa mshirika muhimu wa Russia. Lukashenko alisema katika kikao na waandishi habari: "Kama shambulio la Russia lingecheleweshwa kwa muda mfupi tu, Ukraine ingetoa pigo kubwa katika ardhi ya Russia."

Ni siku 50 sasa tangu vita vya Ukraine vianze na hadi sasa nchi 25 zimeitumia Kyiv silaha mbalimbali za kijeshi. Warussia wametangaza wazi kuwa hawakusudii kuikalia kwa mabavu Ukraine. Tangu kuanza vita hivyo, nchi za Magharibi zimeipatia Ukraine shehena kubwa ya silaha, lakini mdhamini mkuu wa silaha za kijeshi kwa Ukraine ni Marekani.

Mbali na msaada wa kijeshi uliotangazwa hapo awali, Rais Joe Biden wa Marekani amepanga kuipatia Ukraine silaha mpya zenye thamani ya dola milioni 750. Moscow imekuwa ikionya mara kwa mara kuwa kutumwa silaha za nchi za Magharibi huko Ukraine kutarefusha muda wa mzozo huo, na hata kuonya kuwa huenda majeshi ya Russia yakazilenga silaha hizo. Joe Biden pia ameanzisha vita vya kisaikolojia na kipropaganda dhidi ya Rais Putin, akimtaja kwa maneno mbalimbali hasi. Biden, kwa mfano, amelitaja shambulio la Putin dhidi ya Ukraine kuwa "mauaji ya kimbari."

Joe Biden amekuwa akiendesha vita vya kipropaganda dhidi ya Putin

Licha ya NATO kudai kuwa haiingilii vita vya Ukraine, lakini ni wazi kuwa Ukraine inapigana vita vya niaba na Russia kwa maslahi ya NATO. NATO inadhamini vifaa na zana za kijeshi, kilojistiki, kijasusi na fedha huku Ukraine ikitakiwa kudhamini nguvu kazi katika vita hivyo. NATO ikiongozwa na Marekani inaamini kwamba madhara ya vita nchini Ukraine, maafa ya askari na uharibifu wa zana za kijeshi katika medani ya vita, pamoja na taathira za vikwazo dhidi ya Russia, hatimaye kutapelekea kuporomoka uchumi wa nchi hiyo na kutilia shaka uhalali wa uongozi wa Rais Putin nchini humo.

Tags