Apr 21, 2022 02:50 UTC
  • Kukosolewa unafiki wa Marekani kuhusu suala la haki za binadamu

Ilhan Omar, mbunge wa Kiislamu katika Congress ya Marekani amesema kuwa madai yanayotolewa na utawala wa Wadhington kuhusu haki za binadamu duniani ni ya kinafiki, na kusisitiza kuwa kama nchi hiyo inataka kuishtaka Russia katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kuhusiana na tuhuma zinazotolewa dhidi yake kuhusu vita vya Ukraine, inapasa kwanza yenyewe ijiunge na kuwa mwanachama wa mahakama hiyo.

Ilham Omar amesema: 'Ni unafiki mkubwa kwa Marekani kutaka uchunguzi wa jinai za kivita huko Ukraine ufanyike dhidi ya Russia katika hali ambayo yenye inapinga uwepo wa mahakama hiyo.' Huku akiwasilisha bungeni siku ya Alhamisi mswada wa kutaka Marekani ijiunge na mahakama ya ICC, Ilham Omar amesema njia bora zaidi ya kuunga mkono uchunguzi dhidi ya Russia kuhusu tuhuma zinazotolewa dhidi yake kuhusiana na vita vya Ukraine ni kwa Marekani kuwa mwanachama wa mahakama hiyo.

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ilibuniwa mwaka 2002 kwa mujibu wa hati ya Rome kwa ajili ya kuchunguza na kufuatilia uhalifu wa kimataifa, yaani mauaji ya kizazi, jinai dhidi ya binadamu, uhalifu wa kivita na ubakaji na kuchukua hatua za kuzuia kukaririwa uhalifu huo. Licha ya Marekani kuhudhuria vikao vya kuasisi mahakama hiyo ambavyo vilifanyika mjini Rome mwaka 1998, lakini ilikataa kupitisha mswada wa kuanzishwa mahakama hiyo na kuendelea kutekeleza vitendo ambavyo vinakwenda kinyume na malengo ya mahakama hiyo ya kimataifa.

Askari wa Marekani walihusika na jinai kubwa za kivita Afghanistan

Ni wazi kuwa Marekani ilikataa kujiunga na Mahakama ya ICC ili kukwepa kufuatiliwa kisheria kutokana na uhalifu mkubwa wa kivita inaofanya katika pembe tofauti za dunia zikiwemo nchi za Afganistan na Iraq. Katika kipindi cha utawala wake huko Marekani, Donald Trump hata aliwawekea vikwazo maafisa wa ngazi za juu wa ICC akiwemo mwendesha mashtaka wake mkuu, kwa kisingizio cha kutaka kuanzisha uchunguzi kuhusu uhalifu na jinai za kivita zilizofanywa na askari wa Marekani huko Afghanistan. Maafisa wa utawala wa Trump walitumia visingizio tofauti vikiwemo vya eti 'tishio dhidi ya utawala wa Marekani' na Washington 'kutokuwa mwanachama' wa mahakama hiyo kwa ahili ya kuhalalisha hatua hiyo isiyo ya kisheria.

Kisingizio kingine kilichotumika ni kuwa, sheria za mahakama hiyo haziendani na sheria za kimataifa. Kwa kutilia maanani kwamba Mahakama ya Kimataifa ya ICC ndiyo marejeo makuu zaidi ya kisheria kimataifa ambayo yamepewa jukumu la kufuatilia uhalifu wa kivita na kibinadamu duniani, inashangaza kuona kwamba viongozi wa utawala wa Trump walijipa madaraka ya kukosoa uhalali wa mahakama hiyo na kudai kwamba haikufaa kufuatilia jinai zilizotekelezwa na askari wa Marekani nchini Afghanistan.

Hivi sasa Marekani inadai kwamba Russia imehusika na jinai za kivita huko Ukraine, ambapo Rais Joe Biden wa nchi amemtuhumu wazi wazi Rais Vladimir Putin wa Russia kuwa ni mhalifu wa kivita  na kutaka ahukumiwe yeye na viongozi wengine wa nchi hiyo kwa makosa ya kivita nchini Ukraine. Suala hilo kwa mara nyingine limeweka wazi unafiki unaofanywa na Marekani kuhusiana na suala zima la haki za binadamu na juhudi zake za kujaribu kuitumia vibaya mahakama ya ICC kwa madhumuni ya kufikia malengo yake haramu katika pembe tofauti za dunia.

Sehemu ya maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi na ukiukaji wa haki za binadamu Marekani

Katika uwanja huo, Andranik Migranyan, mjuzi wa masuala ya kisiasa anasema: 'Marekani inakiuka haki za binadamu kuliko nchi nyingine yoyote ulimwengu." Hali mbaya ya haki za binadamu na ubaguzi unaofanywa na serikali ya Washington dhidi ya raia weusi wa nchi hiyo na vilevile vitendo vya mabavu na ukatili unaotekelezwa dhidi yao na polisi ya nchi hiyo unaanika wazi uongo wa madai yanayotolewa na viongozi wa Washington kuhusu suala la haki za binadamu. Rekodi mbaya na jinai za kutisha zinazofanywa na nchi hiyo katika pembe tofauti za dunia, na hasa Guantanamo, Vietnam, Afghanistan, Iraq na Syria zinaweka wazi madai ya kinafiki ya Marekani kuwa inaheshimu na kutetea haki za binadamu ulimwenguni.

Tags