Apr 25, 2022 08:36 UTC
  • Macron ashinda uchaguzi wa rais wa Ufaransa

Emmanuel Macron jana Jumapili, Aprili 24, alichaguliwa tena katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais kuiongoza Ufaransa, na hivyo kuchukua hatamu za nchi hiyo kubwa ya Ulaya kwa kipindi kingine cha miaka 5.

Kwa mujibu wa matokeo ya awali ya uchaguzi huo, Macron amepata zaidi ya asilimia 58 ya kura, huku mpinzani wake, Marine Le Pen wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha National Rally, akipata asilimia 42. Baada ya kutangazwa matokeo hayo Le Pen amekiri kushindwa na kusema: "Leo tutaanza kampeni kubwa kwa ajili ya uchaguzi wa wabunge."

Takriban Wafaransa milioni 48.7 walitimiza masharti ya kupiga kura ambapo asilimia 62 miongoni mwao walijitokeza kupiga kura. Kura nyeupe katika uchaguzi wa jana wa rais wa Ufaransa zifikia asilimia 28, kiwango cha juu ambacho hakijawahi kushuhudiwa nchini humo tangu 1969. Suala jingine muhimu la kuashiria kuhusiana na uchaguzi wa rais wa Ufaransa ni idadi ndogo ya raia waliojitokeza, jambo ambalo linaonyesha kutoridhishwa sehemu kubwa ya watu wa Ufaransa na hali ya sasa ya nchi hiyo.

Suala la nani angeshinda baina ya Macron au Le Pen katika duru hii ya uchaguzi lilikuwa nyeti sana ndani ya Ufaransa na barani Ulaya kwa ujumla. Kwa sababu, kuchagua kila mmoja wa wagombea hawa wawili na kupata tiketi ya kuingia ikulu ya Elysee kunaainisha njia tofauti kwa Wafaransa na Ulaya. Kwa kuzingatia misimamo mikali ya Marine Le Pen anayepinga baadhi ya sera za Ulaya, kuchaguliwa kwake kungezidisha sera na sheria za kupiga vita uhamiaji na kushadidisha mashinikizo kwa Waislamu nchini Ufaransa.

Misikiti mingi imefungwa nchini Ufaransa katika utawala wa Macron

Katika ngazi ya Ulaya pia, kushinda Le Pen katika uchaguzi wa jana kungeifanya Ufaransa ijitenge na Umoja wa Ulaya na kukaribiana zaidi na madola kama Russia na China. 

Kwa upande mwingine, kuchaguliwa Emmanuel Macron kuwa rais wa Ufaransa, tunatoa dhamana ya kuendelezwa sera na siasa za sasa ndani ya nchi; na katika uga wa nje, Ufaransa, pamoja na nchi nyingine za Ulaya, zitafuata mkondo uleule wa kuzidisha mashinikizo dhidi ya Russia.

Bila shaka, Marekani pia imefurahishwa na ushindi wa Macron, kwa sababu inaweza kuwa na uhakika kwamba itaendelea kuungwa mkono na Paris katika kampeni kubwa ya sasa dhidi ya Russia. 

Sera za serikali ya Macron katika miaka 5 iliyopita zimesababisha maandamano makubwa ya kijamii, ikiwa ni pamoja na kuibuka kwa harakati ya Vizibao vya Njano, ambayo inapinga vikali hali ya sasa ya kiuchumi na kijamii nchini Ufaransa.

Ukweli ni kwamba wapiga kura wengi wa Ufaransa waliompigia kura Macron hawakufanya hivyo kwa sababu ya kuridhishwa na sera na siasa zake, bali kwa kutaka Marine Le Pen asichaguliwe kuwa rais wa nchi hiyo. Kwa maneno mengine ni kuwa, Wafaransa hawakumchagua Macron kwa sababu ya kumpenda, bali kwa sababu ya kumchukia Marine Le Pen. Wiki chache kabla ya duru ya pili ya uchaguzi wa rais wa Ufaransa, kuliibuka wimbi kubwa katika jamii ya Wafaransa, wakiongozwa na vuguvugu la Vizibao vya Njano, ambalo lilitaka raia wa nchi hiyo wasishiriki katika uchaguzi kwa kauli mbiu "Si Macron Wala Le Pen". Kuhusiana na hilo wananchi wa Ufaransa wamefanya maandamano kadhaa katika siku za hivi karibuni wakitoa wito wa kususiwa duru ya pili ya uchaguzi wa rais wa Ufaransa. Wafaransa wanawaona Macron na Le Pen kuwa hawafai kushika hatamu za kuongoza nchi hiyo. 

Ufaransa baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa rais

Jambo muhimu linaloonyesha kutoridhika kwa Wafaransa na hali ya sasa ni maandamano yaliyotokea baada tu ya uchaguzi wa jana. Muda mfupi baada ya kutangazwa matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais wa Ufaransa, maelfu ya waandamanaji walimiminika barabarani wakipinga ushindi wa Macron, jambo ambalo limesababisha makabiliano na polisi.

Tags