Apr 27, 2022 02:38 UTC
  • Changamoto za ndani na za nje za Macron katika duru ya pili ya urais nchini Ufaransa

Kushinda tena Emmanuel Macron Rais wa Ufaransa katika uchaguzi wa Rais wa mwaka huu kumeibua maswali mengi kuhusiana na sababu hasa ya wananchi wa nchi hiyo kumpigia kura mwanasiasa huyo.

Sambamba na hilo, katika miaka mingine mitano ya uongozi Macron atakabaliwa na changamoto nyingi za ndani na za nje.

Weledi wa mambo wanasema kuwa, kwa kuzingatia kwamba, Macron ameibuka na ushindi wa asilimia 58 mkabala na asilimia 42 ya mpinzani wake mkuu na mkongwe Marine Le Pen, kimsingi kiongozi huyo ni mwakilishi wa asilimia 38 tu ya wananchi wa Ufaransa waliotimiza masharti ya kupiga kura na mwakilishi wa asimilia 27 ya wananchi wa nchi hiyo ya bara Ulaya.

Chunguzi na tathmini mbalimbali zilizofanyika kabla ya uchaguzi huo, nazo kwa kiwango kikubwa zinanashabihiana na matokeo haya. Hata hivyo Macron mwenyewe amekiri kwamba, sehemu ya kura alizopata katika duru ya pili ya uchaguzi huo alipigiwa na wapiga kura ambao nia yao ilikuwa ni kuzuia Marine Le Pen asishinde kiti hicho.

Ukweli wa mambo ni kuwa, Wafaransa walikuwa na machaguo mawili ambayo ni baya na baya zaidi, hivyo hawakuwa na budi ghairi ya kuchagua chaguo baya mbele ya chaguo baya zaidi. Jean-Luc Melenchon, mmoja wa wanasiasa wa mrengo wa kushoto ambaye alishika nafasi ya tatu katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais amesema katika radiamali yake kwa ushindi wa Macron kwamba, Macron ni rais mbayya kabisa wa tano wa Ufaransa ambaye ameogolea katika bahari ya kura za kujizuia, nyeupe na batili.

Rais Macron (kushoto) na Marine Le Pen

 

Pamoja na hayo suala muhimu baada ya kuibuka mshindi Macron na kushika tena hatamu za uongozi nchini Ufaransa ni changamoto za ndani na nje zinazomkabili mwanasiasa huyo kijana. Katika uga wa ndani, changamoto kubwa zaidi inayoikabili serikali ya Macron ni namna ya kukabiliana na virusi vya corona kwa upande mmoja na kuchukua hatua za kuboresha uchumi wa nchi hiyo kwa upande wa pili.

Wakati huo huo, kuendelea kushuhudiwa wimbi la malalamiko dhidi ya sera za mipango ya kiuchumi na kijamii ya serikali ya Macron kutokana na kuenea virusi vya corona na athari ya vita vya Ukraine, ni mambo ambayo yameifanya serikali yake kukabiliwa na hali mbaya zaidi. Upinzani dhidi ya serikali ya Macron uliingia katika hatua mpya mwaka 2018 baada ya kuundwa Harakati ya Vizibao vya Njano.

Katika duru ya kwanza ya uongozi wake, Rais Macron alikabiliwa na malalamiko mengi kama marekebisho ya sheria ya kazi, mfumo wa kustaafu, sheria za kodi pamoja na kanuni zinazohusiana na kukabiliana na corona na maradhi ya Covid-19. Harakati ya Vizibao vya Njano nayo ilitoa pigo kubwa kwa serikali ya Macron ambapo rais huyo kijana wakati mwingine alilazimika kukubali baadhi ya matakwa yao ili ni kupunguza malalamiko dhidi ya serikali yake.

Changamoto nyingine inayomkabili Macron ni suala la wahajiri na wakimbizi na vilevile juhudi zake mtawalia za kudhibiti Waislamu kadiri inavyowezekana ambao wanahesabiwa kuwa jamii ya walio wachache nchini Ufaransa. Hii ni katika hali ambayo, Ufaransa ndio yenye jamii kubwa zaidi ya Waislamu barani Ulaya.

 

Katika uga wa nje pia ushindi wa Emmanuel Macron umepokewa kwa mikono miwili na Marekani na madola ya Ulaya na viongozi wa madola hayo wanaona kuwa hiyo ni ishara ya wazi kwamba, ushindi huo ni hatua nyingine moja mbele katika uga wa kuweko uthabiti katika Umoja wa Ulaya, demokrasia duniani na kukabiliana na Russia.

Katika kipindi cha sasa, changamoto kubwa zaidi ya nje ya Macron ni Waislamu, kuendelea vita vya Ukraine na utendaji wa Paris katika uwanja huo. Kabla ya kutokea vita hivyo, Macron alifanya safari mara kadha nchini Russia ambapo sambamba na kufanya mazungumzo mara kadhaa kwa njia ya simu na Rais Vladimir Putin wa nchi hiyo akiwa na lengo la kuzuia hujuma ya kijeshi ya Moscow dhidi ya Ukraine ili kwa njia hiyo aongeze kukubalika na kupendwa za fikra za waliowengi nchini Ufaransa na barani Ulaya kwa ujumla.

Pamoja na hayo baada ya Russia kutekeleza kivitendo hujuma na mashambulio yake ya kijeshi dhidi ya Ukraine imefahamika kwamba, kimsingi Putin hakuuupa umuhimu upatanishi wa Macron. Hili lilikuwa ni pigo kwa Rais huyo wa Ufaransa. Hivi sasa Ufaransa ikiwa katika fremu ya kambi ya waitifaki wa Marekani imesimama kukabiliana na Russia.

Siyo tu kwamba, Ufaransa imetekeleza vikwazo na kuzuia mali za Russia, bali imekuwa mstari wa mbele na amilifu katika kuipatia Ukraine misaada ya kijeshi na silaha. Sambamba na hayo, Ufaransa ikiwa pamoja na mataifa ya Ulaya Mashariki ambayo ni wanachama wa Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Kijeshi ya Nchi za Magharibi NATO imeunga mkono vikwazo vya mafuta dhidi ya Russia.

Tags