May 01, 2022 14:31 UTC
  • Misimamo ya Taliban mkabala wa mlipuko wa kigaidi huko Kabul

Msemaji wa serikali ya Taliban amelaani shambulizi la kigaidi lililolenga msikiti mmoja katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul siku ya Ijumaa iliyopita. Kundi la Taliban limelitaja shambulizi hilo ambalo liliua na kujeruhi makumi ya waumini, kuwa ni uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Makumi ya watu waliuawa shahidi na kujeruhiwa katika shambulio la kigaidi lililotokea kwenye Msikiti wa Khalifa mjini Kabul.

Msemaji wa Taliban, Zabihullah Mujahid ametuma ujumbe kwenye mtandao wa Twitter akilaani shambulio la kigaidi la Kabul na kusema: "Shambulio hili lililofanyika wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, ni uhalifu dhidi ya ubinadamu, na vitendo kama hivyo havina uhusiano wowote na Uislamu na ubinadamu." Mujahid ametoa pole kwa familia za wahanga wa shambulio hilo la kigaidi na kusisitiza kuwa, wahusika wa jinai hiyo watakamatwa na kuadhibiwa.

Zabihullah Mujahid

Hujuma hiyo inafuatia ile ya siku ya Alhamisi iliyopita iliyolenga msikiti wa Wislamu wa madhehebu ya Shia katika mji wa Mazar-i-Sharif, makao makuu ya mkoa wa Balkh mbapo watu 9 waliuawa na wengine 13 kujeruhiwa katika milipuko miwili mfululizo.

Shambulio la kigaidi dhidi ya Msikiti wa Waislamu wa madhehebu ya Suni wa Khalifa mjini Kabul limeonesha kuwa, magaidi wa Afghanistan kwa wakati mmoja wamezilenga jamii za Shia na Suni na kwamba ugaidi katika nchi hiyo unahatarisha usalama wa makundi yote ya kidini.

Kuongezeka mashambulio ya kigaidi nchini Afghanistan hasa katika mji wa Kabul ambako serikali ya Taliban imebakia kama mtazamaji tu wa vitendo hivyo viovu na vya kinyama, ni ishara isiyo na shaka ya udhaifu wa kundi hilo na kutoweza kudhamini usalama na kukabiliana na makundi ya kigaidi.

Kwa kutilia maanani kuwa katika miezi ya hivi karibuni na chini ya utawala wa Taliban nchini Afghanistan, kundi la kigaidi la ISIS limetangaza kuwa limehusika kupanga na kutekeleza mashambulizi mengi ya kigaidi nchini humo, kunaonekana udharura wa serikali ya Taliban kukabiliana ipasavyo na kundi hilo la kigaidi. Vilevile kwa kuzingatia kuwa serikali ya Taliban inajua vyema kwamba ISIS ndilo kundi kuu linalovuruga amani na usalama nchini humo, kutochukuliwa hatua madhubuti za kukabiliana na kundi hilo la kigaidi kunazusha swali muhimu ambalo bado Taliban hawajalijibu.

Hata hivyo na licha ya matakwa ya kitaifa nchini Afghanistan ya kuwepo utulivu na usalama na kuchukua hatua za kulidhibiti kundi la kigaidi la ISIL, msimamo wa serikali ya Taliban kuhusu kundi hilo umezusha mjadala mkubwa. Serikali ya Taliban inapuuza uhalifu na mauaji ya kinyama ya kundi hilo ikidai kuwa ISIL sio tishio kubwa kwa Afghanistan. Hii ni licha ya kwamba, mashambulizi ya kigaidi ya ISIL katika wiki za hivi karibuni katika maeneo tofauti ya Afghanistan yamesababisha vifo vya mamia na kujeruhiwa wengine wengi.

Msimamo laini wa serikali ya Taliban mkabala wa mashambulizi ya ISIL nchini Afghanistan kwa namna fulani umeibua hasira na hisia kali za wananchi kuhusiana na msimamo wa kundi hilo mbele ya vitendo vya kikatili na vya Daesh.

Athari za hujuma ya Daesh dhidi ya Waislamu katika msikiti wa Waislamu wa madhehebu ya Shia, Mazar-i-Sharif.

Kwa sasa Waafghani wanajiuliza kwamba, ni kwa nini kundi la Taliban, tofauti na kipindi cha kuwepo kwa majeshi ya kigeni nchini Afghanistan kati ya mwaka 2001 na 2021, halikabiliani ipasavyo na Daesh na makundi mengine yanayovuruga utulivu nchini humo, na badala yake limekuwa mtazamaji tu mbele ya mashambulizi hayo ya kigaidi?

Mwenendo huo wa serikali ya Taliban wa ulegevu na kutochukua hatua za kukabiliana na mashambulizi ya kigaidi ya ISIL nchini Afghanistan, ambayo yameshika kasi katika wiki na siku za hivi karibuni, umewafanya Waafghani wasiwe na imani kwa utawala wa Taliban.

Tags