May 04, 2022 02:35 UTC
  • Putin atia saini amri ya kuziwekea vikwazo nchi za Ulaya na Marekani

Ikulu ya Russia (Kremlin) imetangaza kuwa, Rais Vladimir Putin wa nchi hiyo ametia saini amri ya kuchukuliwa hatua kali za kulipiza kisasi vikwazo vilivyowekwa na nchi za Magharibi dhidi ya Moscow.

Msemaji wa Ikulu ya Russia, Dmitry Peskov amewaambia waandishi wa habari kuwa, amri hiyo ya Rais Vladimir Putin imezipa wizara za Russia muda wa siku 10 kukusanya orodha ya nchi na watu ambao watawekewa vikwazo hivyo ikiwa ni kulipiza kisasi cha vikwazo ambavyo nchi za Ulaya na Marekani zimeiwekea Moscow.

Hatua hiyo ya Rais wa Russia imechukuliwa katika hali ambayo tangu tarehe 24 Februari vilipoanza vita vya Ukraine nchi hizo za Magharibi hazijachukua hatua yoyote ya kupunguza wasiwasi ilio nao Moscow wa kujitanua kijeshi nchi za Ulaya na Marekani kwenye mipaka ya Russia. Nchi hizo za Magharibi zimeiwekea vikwazo vikubwa Moscow kwa shabaha ya kuifanya itengwe kimataifa na kuvuruga uchumi wake.

Nchi za Magharibi hasa za Ulaya ni tegemezi mno kwa nishati ya Russia

 

Mawaziri wa nchi za Ulaya wamepanga kuitisha kikao ili kuchunguza njia nyingine za kuchukua dhidi ya Moscow, hatua ambayo imepokewa kwa onyo kali na Russia.

Kwa mujibu wa amri mpya ya Rais Vladimir Putin wa Russia, viongozi wa nchi hiyo watapigwa marufuku kushirikiana kwa njia yoyote ile na mashirika na watu wa nchi za Ulaya na Marekani watakaokuwemo kwenye orodha hiyo itakayoainishwa kwenye vikwazo vipya vya Russia.

Ikumbukwe kuwa nchi za Magharibi hasa za Ulaya ni tegemezi mno kwa nishati ya bei nafuu ya Russia na kuna hatari ya kusambaratika uchumi, kutokea mfumuko mkubwa wa bei na kupanda sana gharama za maisha katika nchi za Ulaya na Marekani.

Tags