May 05, 2022 02:15 UTC
  • Rais Vladimir Putin wa Russia
    Rais Vladimir Putin wa Russia

Ikulu ya Kremlin imetangaza Jumanne kuwa, Rais Vladimir Putin wa Russia ametia saini amri ya kukabiliana na 'hatua zisizo za kirafiki za baadhi ya nchi za kigeni na mashirika ya kimataifa." Dikrii hiyo inasisitiza hatua za kulipiza kisasi dhidi ya nchi ambazo zimetajwa kuwa 'zisizo za kirafiki'. Kwa mujibu wa amri hiyo Russia itaziwekea vikwazo baadhi ya nchi na taasisi za kimataifa.

Putin ameiamuru serikali ya Russia pia itayarishe katika kipindi cha siku 10 orodha ya watu ambao watawekewa vikwazo hivyo vya ulipizaji kisasi.

Amri hiyo ya Putin ina maana kuwa nchi hiyo itasitisha uuzaji wa mali zake ghafi kwa nchi, taasisi au watu waliowekewa vikwazo. Hali kadhalila dikrii hiyo ya Putin inayapa mashirika ya Russia idhini ya kukiuka mikataba ambayo ilikuwa imesainiwa na waliowekewa vikwazo.

Hatua hii imekuja katika hali ambazo Josep Borrell, mkuu wa sera za kigeni katika Umoja wa Ulaya alitangza Jumanne, katika siku ya 69 ya oparesheni ya kijeshi ya Russia nchini Ukraine kuwa, umoja huo unatayarisha kifurushi cha sita cha vikwazo dhidi ya Russia. Inatazamiwa kuwa vikwazo hivyo vya Umoja wa Ulaya vitajumuisha kufutwa taratibu uagizaji mafuta ya petroli kutoka Russia kwa asilimi 30.

Inaelekea kuwa, vita vya vikwazo baina ya Russia na kambi ya Magharibi vimeingia katika duru mpya ambapo Moscow inaonekana kuwa na mbinu nyingi za vikwazo ambavyo itatumia dhidi ya Wamagharibi.

Russia ni mzalishaji mkubwa wa bidhaa mbili za kistratijia duniani yaani gesi na mafuta ya petroli. Kwa kuzingatia kuwa nchi za Ulaya zinategemea sana bidhaa hizi mbili za kistratijia inaonekana Moscow itatumia uwezo wake huo katika sekta hii kadiri inavyoweza ili kuzishinikiza nchi za Ulaya hasa zile ambazo zinashirikiana na Marekani katika kuiwekea vikwazo. Nchi za Ulaya sasa ziko mbioni kupunguza utegemezi wao wa mafuta na gesi ya Russia kwa lengo la kuinyima Moscow pato linatokana na uuzaji wa bidhaa hizo mbili. Pamoja na hayo inasemekana kuwa tokea vita vianze Ukraine zaidi ya miezi miwili iliyopita,  Russia imeuza mafuta yenye thamani ya takribani dola bilioni 60. Hata kama nchi zinazouza mafuta kwa wingi duniani zinaweza kwa kiasi fulani kujaza pengo la mafuta ya Russia lakini jambo lililo wazi ni kuwa kukosekana mafuta ya Russia katika soko la kimataifa kunaweza kusababisha ongezeko kubwa la bei ya bidhaa hiyo.

 Scott  Sheffield mkurugenzi wa shirika kubwa la mafuta la Marekani) la Pioneer Natural Resources alisema mwezi Machi kuwa njia pekee ya kumshinda Putin ni kuwekea vikwazo mafuta na gesi ya Russia. Hata hivyo alionya kuwa iwapo Russia itawekewa vikwazo vya mafuta na gesi, bei ya mafuta ghafi ya petroli duniani itapindukia dola 200 kwa pipa.

Nchi za Ulaya ni tegemezi sana kwa Russia katika sekta ya gesi kuliko mafuta au petroli. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2020, nchi za Ulaya hutegemea sana gesi ya Russia ambapo nchi kama Jamhuri ya Check inategemea gesi ya Russia kwa asilimia 100. Ujerumani nayo ambayo ina uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya ina utegemezi wa asilimia 66 kwa gesi ya Russia. Ingawa nchi za Ulaya zinataka kupunguza utegemezi wao kwa Russia  lakini machakato huo utachukua muda mrefu na utagharimu kiasi kikubwa cha fedha. Ni kwa msingi huo ndio baadhi ya nchi za Ulaya kama vile Hungary zinapinga vikwazo dhidi ya Russia. Mbali na sekta hiyo ya nishati, Russia pia ni muuzaji mkubwa wa fatalaiza, ngano, mahindi, shayiri na mbegu za mafuta ya kupikia.

Hivyo amri ya Putin ya kuziwekea vikwazo nchi za Ulaya na Marekani na pia nchi zingine za dunia zilizojiunga na kambi hiyo ya Magharibi ni jambo ambalo litakuwa na taathira hasi sana kwa uchumi wa dunia. Si tu kuwa kuna uwezekano wa kupungua bidhaa zilizowekewa vikwazo katika soko la dunia bali pia bei za bidhaa hizo zitaongezeka zaidi duniani. Kimsingi kile ambacho Putin anataka kuzifahamisha nchi za Magharibi ni kuwa, vikwazo ni upanga wenye ncha mbili na iwapo nchi za Magharibi zimeiwekea Russia vikwazo ambavyo havijawahi kushuhudiwa, sasa umewadia wakati wa Russia nayo kuziwekea vikwazo vikali nchi ambazo imezitaja kuwa si rafiki.

Tags