May 06, 2022 02:37 UTC
  • Kuongezeka upinzani barani Ulaya dhidi ya kuwekewa vikwazo vya mafuta Russia

Licha ya vitisho vya Umoja wa Ulaya kuhusiana na kuiwekea vikwazo vya mafuta Russia katika fremu ya kifurushi cha sita cha vikwazo dhidi ya nchi hiyo, lakini jambo hilo linaonekana kukabiliwa na upinzani mkali barani humo na hata baadhi ya viongozi wa Marekani kutoa onyo dhidi ya hatua hiyo.

Richard Sulik, Waziri wa Uchumi wa Slovakia alionya Jumatano iliyopita kuhusiana na kuwekewa vikwazo vya mafuta nchi ya Russia. Waziri Richard amesema: Kupiga marufuku uingizwaji wa mafuta ya Russia barani Ulaya, kutasambaratishha kabisa uchumi wa bara hilo sambamba na kuziathiri pakubwa nchi za Slovakia, Austria, Jamhuri ya Czech na Ukraine.

Péter Szijjártó, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Hungary naye amekosoa misimamo hasi ya Ulaya na kueleza kwamba, nchi yake inaandamwa kidhulma na viongozi wa mataifa ya Umoja wa Ulaya kutokana na misimamo yake kuhusiana na kujidhaminia vyanzo vya nishati yaani gesi na mafuta kutoka Russia.

Katika radiamali yake kwa uokosoaji wa madola ya Ulaya dhidi ya Hungary kutokana na kuwa tegemezi nchi hiyo kwa Russia katika kukidhi mahitaji yake ya mafuta na gesi amesema: Kuhusiana na jambo hili, tunachozingatia sisi ni maslahi ya kitaifa ya Hungary, wala hatuna hamu ya kutaka kujua Magharibi na Mashariki wanafikiria nini. Usalama wa kweli ni sisi kujidhaminia nishati na hili ni jambo lenye umuhimu kwetu, kwani mzunguko wa uchumi wa Hungary hauzunguki pasi na kuingiza mafuta kutoka Russia na kukata utegemezi kwa vyanzo wa nishati vya Russia ni jambo ambalo ambalo kwetu haliwezekani.

Rais Putin wa Russia ametia saini amri ya kuiwekea vikwazo vya ulipizaji kisasi kambi ya Magharibi

 

Kwa upande wake, Janet Yellen Waziri wa Fedha wa Marekani alitangaza siku ya Jumatano kwamba, hatua ya Umoja wa Ulaya ya kuiwekea Russia vikwazo vya mafuta yumkini ikaongeza bei ya mafuta ghafi. Aliongeza kuwa, kuna haja ya kuutafutwa njia mbadala ya kuiwekea vikwazo Russia bila ya kuweko matokeo mabaya na hasi ya kupanda bei ya mafuta katika soko la dunia.

Inaonekana kuwa, hakuna maafikiano na mtazamo mmoja barani Ulaya kuhusiana na kuiwekea vikwazo vya mafuta Russia. Ukweli wa mambo ni kuwa, kundi la nchi ambazo zina utegemezi kwa mafuta ya Russia siyo jambo jepesi kwao kuweka kando hilo na kisha kutafuta chaguo jingine. Jambo hilo haliwezekani kufanyika hususan katika kipindi cha muda mfupi na hilo linaweza kuwa na hasara kubwa kwa uchumi wao.

Msimamo wa Waziri wa Uchumi wa Slovakia na kusema kwake bayana kwamba, kuiwekea Russia vikwazo vya mafuta kutasambaratisha uchumi wa Ulaya ni ishara ya wazi kuhusu nukta hii.

Mkabala na nchi hizo, kuna kundi la mataifa ambayo ni waitifaki wa Marekani ambayo yamekuwa yakishinikiza Russia kuwekewa vikwazo vya mafuta. Baadhi ya mataifa hayo ni Uingereza, Poland na mataifa ya Ukanda wa Baltic.

Liz Truss, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uingereza

 

Liz Truss, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uingereza ametoa wito wa kuzuiwa uingizaji wa nishati kutoka Russia yakiwemo mafuta na gesi. Katika matamshi yake yaliyo dhidi ya Russia, Liz Truss amesema: Vita nchini Ukraine ni vita vyetu na ni vita vya wote. Tumeazimia kushirikiana na washirika wetu kwa ajili ya kuandaa mpango mpya wa kuiunga mkono Ukraine.

Mintarafu hiyo inaonekana kuwa, filihali Ulaya ipo katika njia panda mbili. Njia ya kwanza ni kuchagua maslahi yao ya kiuchumi na hivyo kuendelea kuingiza mafuta na gesi barani humo kutokea Russia na kwa msingi huo kustawisha uchumi na kuzuia kujitokeza hasara kubwa kwa mataifa hayo. Chaguo la pili ni kuungana na Marekani katika fremu ya malengo makubwa ya kijiopolitiki ya Magharibi yaani kukabiliana na nguvu za kimataifa ambazo zinataka kuweko mabadiliko katika nidhamu ya sasa hususan Russia na katika hatua ya pili China.

Christian Lindner, Waziri wa Fedha ya Ujerumani anasema: Vita vya Ukraine na Russia vitapelekea kutokea mfumo mpya katika dunia.

 

Kauli hizi zinaonyesha wazi kwamba, madola mengi ya Ulaya ambayo hivi sasa yapo katika kambi ya kuiunga mkono Ukraine na yamejiunga katika safu ya kuiwekea vikwazo Russia yameamua kuwa pamoja na Marekani na malengo ya kijiopolitiki ya Magharibi.

Pamoja na hayo, upinzani wa mataifa kama Slovakia na Hungary kwa uamuzi wa Umoja wa Ulaya kuhusiana na suala la kuiwekea vikwazo vya mafuta Russia ni jambo linaloonyesha kuwa, ndani ya Ulaya hakuna msimamo na mtazamo mmoja kuhusiana na hatua hiyo; kwani baadhi ya mataifa ya bara hilo hayako tayari kuyatoa muhanga maslahi yao ya kitaifa kwa ajili ya maslahi na malengo makubwa ya Marekani.

Tags