May 08, 2022 12:16 UTC
  • Kiongozi wa Taliban atoa agizo jipya kuhusu Hijabu kwa wanawake wa Afghanistan

Kiongozi Mkuu wa Taliban nchini Afghanistan Haibatullah Akhunzada ametoa agizo lenye vipengee vinne la sheria mpya kuhusu mipaka ya vazi la Hijabu kwa wanawake wa nchi hiyo.

Kundi la Taliban, ambalo lilitwaa hatamu za madaraka ya nchi Agosti 15, 2021 liliahidi kuwa litakuwa na mitazamo ya wastani katika kuchunga haki za binadamu na haki za wanawake kulinganisha na kipindi cha mwanzo cha utawala wake kuanzia mwaka 1996 hadi 2001.

Hata hivyo baadhi ya weledi wa mambo wanaitakidi kuwa, Taliban imeanza hatua kwa hatua kubana haki za Waafghani hasa wanawake, ikiwemo kuwazuia watoto wa kike kurudi maskulini na kutowaruhusu wanawake kufanya kazi katika sekta nyingi za serikalini.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, kulingana na amri iliyotolewa na Kiongozi wa Taliban na ambayo imesomwa katika kikao kilichoitishwa katika Wizara ya Kuamrisha Mema na Kukataza Maovu ya serikali ya muda ya kundi hilo, wanawake wote wanalazimika kuvaa hijabu, ikiwemo kufunika nyuso zao wanapokuwa katika hadhara na kwamba watakaohalifu kufanya hivyo watachukuliwa hatua kali.

Wanawake wa Afghanistan wakiwa wamevalia buibui aina ya Burqa

Wizara ya kuamrisha mema na kukataza maovu imesema, kuvaa hijabu ni "lazima" kwa wanawake waliobaleghe na ikafafanua kwamba "aina bora ya hijabu" ni buibui aina ya burqa.

Sheria hiyo imebainisha kuwa, katika hatua ya kwanza itafuatiliwa na kutambuliwa nyumba ya mwanamke asiyevaa hijabu, ambapo baba au walii wake ataelimishwa na kupewa ushauri. Katika hatua itakayofuata, walii wa mwanamke huyo ataitwa ili kusailiwa na katika hatua ya tatu atafungwa kifungo cha siku tatu.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, katika hatua ya nne, walii wa mwanamke atafikishwa mahakamani na kupewa adhabu "inayostahiki".

Wizara ya kuamrisha mema na kukataza maovu ya Taliban imeendelea kubainisha pia kwamba, wanawake wasiovaa hijabu ambao wanafanya kazi katika idara za serikali ya Afghanistan wataachishwa kazi.../

Tags