May 11, 2022 02:39 UTC
  • Kuongezeka idadi ya watu wanaokabiliwa na baa la njaa duniani kufuatia vita vya Ukraine

Baa la njaa limegeuka na kuwa tatizo kubwa linaoukabili ulimwengu katika hali ya hivi sasa.

Kuendelea vita vya Russia na Ukraine kumelifanya tatizo hili lichukue wigo mpana zaidi kiasi kwamba, takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, endapo vita hivyo vitaendelea, basi idadi ya watu wanaokabiliwa na hatari kubwa ya baa la njaa duniani itaongezeka.

Umoja wa Mataifa unaeleza kwamba, kama vita vya Russia na Ukraine vitaendelea basi idadi ya sasa ya watu milioni 47 wanaokabiliwa na njaa kali itaongezeka na kukaribia milioni 323.

Weledi wa mambo wanasema kuwa, vita vya Russia na Ukraine vimesababisha maeneo mengi ya Ukraine kuakhirisha zoezi la kupanda bidhaa za nafaka huku mashamba mengi ya ngano katika nchi hiyo yakigeuka na kuwa medani ya vita. Asasi mbalimbali za kimataifa zimesema katika ripoti zao kwamba, hata usafirishaji nje wa ngano ya Ukraine iliyokuwa imevunwa kabla ya kuanza vita hivyo, umekabiliwa na matatizo makubwa.

Afghanistan ni miongoni mwa mataifa ambayo yanakabiliwa na baa la njaa

 

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) linatabiri kuwa, kwa akali asilimia 20 ya mazao hayo imeshindikana kuyafikia kutokana na sababu mbalimbali kama kutekeketezwa mashamba au kuangamizwa vyanzo vinavyopaswa kutumika kushughulikia mazao hayo.

Si hayo tu, bali akthari ya bandari za Ukraine zimefungwa na hakuna uwezekano wa kusafirisha nje ya nchi mazao yaliyokuwa tayari kwa ajili ya kusafirishwa. Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetoa wito wa kufunguliwa bandari za Ukraine ili akiba ya ziada ya chakula cha nchi hiyo iweze kusafirishwa nje ya nchi na kuwasaidia mamilioni ya watu katika maeneo mbalimbali ya dunia ambao wanataabika kwa njaa.

Hali hiyo inaripotiwa katika hali ambayo, sera za kupenda vita za Marekani na madola ya Ulaya, hatua za Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO), misaada ya silaha ya madola Magharibi kwa Ukraine na kuchochea kuni za moto wa vita hivyo ni hatua ambazo kivitendo zimechangia pakubwa kupanua wigo wa vita hivyo na hata kuchukua muda mrefu.

 

Hii ni katika hali ambayo, hatua ya madola ya Magharibi ya kuiwekea vikwazo vingi Russia imeathiri soko la bidhaa za chakula na nishati katika maeneo mbalimbali ulimwenguni na kuwa sababu ya kupanda bei. Matokeo yake ni hali ya sasa tunayoishuhudia duniani ya kuwa ghali na kuadimika bidhaa za chakula.

Hali hii licha ya kuwa imekuwa na taathira hasi kwa uchumi wa dunia, lakini kuongezeka bei za bidhaa za chakula kumekuwa na taathira kubwa zaidi kwa nchi masikini na zinazokabiliwa na vita kama Yemen.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ni kuwa, bei za bidhaa za chakula ziliongezeka kwa takribani asilimia 75 katikati ya mwaka 2020. Umoja wa Mataifa umeonya kuwa, yumkini bei za vyakula zikaongezeka zaidi ambapo hii ni habari mbaya kwa wale wanaotaabika kwa njaa hivi sasa katika maeneo tofauti ya dunia.

Tathmini ya Kituo cha Maendeleo Duniani inaonyesha kuwa, kuongezeka gharama za maisha kumetokana na vita na vikwazo ilivyowekewa Russia na kwamba, endapo mwenendo huu utaendelea basi kuna uwezekano wa watu wengine milioni 40 kutumbukia katika umasikini shadidi.

Vita vya Ukraine

 

Fauka ya hayo, mbali na kuweko hatari ya uhaba wa bidhaa za chakula kutokana na vita vya Ukraine, wakulima katika maeneo mbalimbali ya dunia wanakabiliwa na matukio mabaya yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi ambayo chimbuko lake ni siasa za kupenda kujitanua za madola Magharibi pamoja na kupuuza kwao masuala yanayohusiana na mazingira.

Ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea katika miongo ya hivi karibuni umesababisha kuangamia mifugo zaidi ya milioni moja katika eneo ya Pembe ya Afrika huku ongezeko la joto duniani likiwa sababu ya ukosefu wa usalama wa chakula katika maeneo tofauti ya duniani ikiwemo Afghanistan. Mazingira haya sambamba na siasa za madola ya Magharibi kuhusiana na Russia na Ukraine yameufanya ulimwengu ukabiliwe na mgogoro mkubwa wa chakula.

Licha ya kuwa madola ya Magharibi yanafanya njama za kuonyesha kuwa, kupanda kwa bei na uhaba wa chakula chimbuko lake ni vita vya Russia na Ukraine, lakini ukweli wa mambo ni kuwa, sera za Wamagharibi za kuingilia na kuchochea kuni za moto wa vita hivyo sambamba na kuiwekea vikwazo Russia hususan sekta ya nishati ya nchi hiyo, zenyewe ni sababu za uhaba wa chakula na kuongezeka idadi ya watu wanaokabiliwa na baa la njaa duniani.

Tags