May 11, 2022 02:40 UTC
  • Singapore yapiga marufuku kuonyeshwa filamu ya Kihindi inayoeneza chuki dhidi ya Uislamu

Serikali ya Singapore imepiga marufuku kuonyeshwa nchini humo filamu ya sinema ya Kihindi inayoeneza chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia).

Waislamu wengi wanaishi Singapore, nchi yenye idadi ya watu wapatao milioni tano na nusu, ambao wengi wao wana asili ya China, Malaysia na India.

Taarifa iliyotolewa na serikali ya Singapore imeeleza kuwa, filamu iitwayo The Files of Kashmir haiwezi kuonyeshwa nchini humo kwa sababu inaweza kuchochea chuki na uadui baina ya jamii mbalimbali na kuvuruga mshikamano wa kijamii na maelewano ya kidini katika jamii ya nchi hiyo ya watu wenye asili na dini tofauti.

Taarifa hiyo imebainisha wazi kuwa, filamu ya The Files of Kashmir inatoa taswira ya kichochezi na ya upande mmoja kuhusu Waislamu sambamba na kujenga picha ya kuonyesha kuwa Wahindu wananyanyaswa na kuudhiwa katila machafuko yanayoendelea hivi sasa katika eneo la Kashmir.

Filamu hiyo inasimulia kisa cha Wahindu waliohajiri kwa umati katika eneo la Kashmir linalokaliwa na India katika muongo wa 1990, wakati ulipoanza muqawama wa mtutu wa bunduki wa Waislamu, ambao ndio waliowengi katika eneo hilo, dhidi ya utawala wa New Delhi.

Imeelezwa kuwa UAE ni nchi Waislamu iliyoruhusu kuonyeshwa filamu hiyo 

Filamu ya The Files of Kashmir ambayo utengenezaji wake umefadhiliwa kifedha na wanasiasa kadhaa wa serikali ya India ya waziri mkuu Narendra Modi, ni moja ya filamu zilizovuma sana katika siku za karibuni nchini humo.

Kutengenezwa kwa filamu hiyo kumeelezewa kuwa ni hatua nyingine katika kampeni za Wahindu wenye misimamo mikali za kueneza chuki zaidi dhidi ya Waislamu wa India.

Wakosoaji wengi wa tasnia ya filamu za sinema wanasema, filamu ya The Files of Kashmir ni wenzo mwingine unaolenga kutoa mbinyo dhidi ya jamii inayobaguliwa ya Waislamu hao.

Modi mwenyewe ameisifu filamu hiyo iliyoanza kuonyeshwa katika kumbi za sinema za India mwezi Machi mwaka huu, akidai kwamba ukweli uliokuwa umefichwa kwa miaka kadhaa sasa umefichuka.../

 

 

 

 

Tags