May 15, 2022 08:00 UTC
  • Imran Khan asema ametishiwa tena kuuawa, arekodi mkanda wa video wa majina ya wahusika

Waziri Mkuu wa Pakistan aliyeuzuliwa Imran Khan amesema, njama za kutishia maisha yake zinaendelea kufanywa ndani na nje ya nchi hiyo na kwamba amesharekodi mkanda wa video wenye majina ya watu wote wanaokula njama dhidi yake.

Akihutubia maelfu ya wafuasi wake katika mji wa Sialkot ulioko mashariki ya jimbo la Punjab, Imran Khan ameeleza kuwa, mpango wa kumuua ungalipo kwenye ajenda ya wanaokula njama dhidi yake na kwamba kitisho hicho dhidi yake kinafuatiliwa ndani na nje ya Pakistan.

Waziri Mkuu huyo wa Pakistan aliyeuzuliwa ameongeza kuwa, amesharekodi mkanda wa video na kuuhifadhi mahala salama na kwamba wakati wowote atakapohatarishiwa maisha yake au kuuawa, mkanda huo utatolewa na kufichua majina na maelezo ya watu wote waliohusika kwenye njama iliyopangwa nje ya nchi dhidi yake na mpango wa kuipindua serikali yake.

Imran Khan alipoapishwa kuwa waziri mkuu wa Pakistan

Aidha amevikosoa vikali vyombo vya ukaguzi vya Pakistan ikiwemo Idara ya Mahakama na serikali ya sasa akiwemo waziri mkuu pamoja na mwanawe ambaye amemtuhumu waziri kiongozi wa jimbo la Punjab kwamba amehusika na ufisadi mkubwa na uhaini dhidi ya nchi.

Imran Khan, alivuliwa wadhifa wa uwaziri mkuu na bunge la Pakistan mwezi uliopita wa Aprili baada ya kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye na kupelekea kuundwa serikali mpya nchini humo.

Ametaka ufanyike uchaguzi wa mapema na kuonya kuwa endapo serikali iliyopo haitatekeleza takwa lake hilo ataitisha maandamano ya mamilioni ya watu kuelekea mji mkuu Islamabad.../

Tags