May 17, 2022 02:26 UTC
  • Wimbi la nchi nzima la chuki ndani ya Marekani; chimbuko na matokeo yake

Baada ya mauaji ya kutisha yaliyofanywa na kijana wa Kizungu kwa sababu ya chuki za ubaguzi wa rangi katika duka kuu la mji wa Buffalo jimboni New York, Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris amesema: "Katika siku hizi, Marekani inashuhudia ueneaji wa chuki nchi nzima."

Hata hivyo tukiitupia jicho historia ya miaka 240 ya Marekani tutabaini kuwa, si kama alivyonena Bi Harris, kwamba "katika siku hizi" nchi hiyo inashuhudia wimbi la nchi nzima la chuki. Siku zote, kumekuwepo na wimbi la chuki za Wazungu dhidi ya Weusi, Weusi dhidi ya Wazungu, Wazungu na Weusi dhidi ya Wahindi Wekundu na chuki za Wahindi Wekundu dhidi ya Wazungu na Weusi. Na baada ya hivi karibuni kuongezeka idadi ya raia wenye asili ya Amerika ya Latini, mihimili hiyo mitatu ya chuki imeongeza mhimili mwingine wa nne.

Pamoja na hayo, wimbi la ueneaji chuki katika jamii ya Marekani si la ubaguzi wa rangi pekee, bali migongano ya kiitikadi na kiidiolojia nayo pia imechangia kuifanya hali iwe mbaya zaidi. Kuna makabiliano ya wanaomwamini Mwenyezi Mungu na walahidi wasio na imani hiyo, Wakristo wa Kiprotestanti mkabala na Wakatoliki, na Wakristo kwa ujumla dhidi ya Waislamu.

Hayo yanajiri katika hali ambayo ufa wa kutisha uliopo kati ya matajiri na masikini ndani ya Marekani umeshadidisha chuki za ubaguzi wa rangi na za kiitikadi katika nchi hiyo. Katika jamii ambayo mtu mmoja peke yake ana utajiri wa zaidi ya dola bilioni 250, huku utajiri wa Wamarekani 400 ukiwa ni sawa na Wamarekani milioni 150; Wamarekani wengine milioni 40 wanaishi chini ya mstari wa umasikini; na kuendelea kwao kuishi kunategemea msaada wa serikali. 

Mabilionea wa Marekani

Ufa na mpasuko huo wa kitabaka unashuhudiwa katika nchi ambayo, raia wake wanaweza kupata na kumiliki kwa urahisi zaidi silaha hatari kuliko hata inavyowagharimu kununua kitabu. Ni kwa sababu hiyo, ndio maana watu wasioridhishwa na hali na mazingira waliyonayo kwa sababu ya rangi ya ngozi zao, kwa sababu za kijamii au hata hali ya nchi yao kwa ujumla, huweza kununua bunduki ya kivita na kuwafyatulia watu risasi na kukatisha maisha yao, bila kujali kama watu hao ni watoto wadogo walioko darasani ndani ya skuli au waumini waliomo kanisani, hekaluni au msikitini.

Wahanga na waathirika wa matukio hayo ya ufyatuaji risasi kiholela wanaweza wakawa hata wapitanjia, kama ilivyotokea Jumapili ya Mei 15 katika duka kuu la mtaa ambao wakazi wake wengi ni Wamarekani weusi katika mji wa Buffalo jimboni New York, ambapo kijana mdogo wa miaka 18 aliyekuwa amejifunga kamera ya video ili kuweza kurusha mubashara kwenye mtandao wa kijamii alichotaka kukifanya, alipowaua kwa kuwapiga risasi watu wasio na hatia yoyote na hatimaye yeye mwenyewe kujisalimisha kwa polisi, akiwaacha watu wengine wamepigwa na butwaa na mshangao.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, kijana huyo Payton S. Gendron alichora juu ya bunduki aliyobeba jina la mwanamke mzungu, ambaye aliuawa katika machafuko ya kibaguzi yaliyotokea Agosti 2020 katika mji wa Kenosha jimboni Wisconsin na akaandika pembeni yake "hiki ni kisasi chako".

Machafuko ya kulalamikia mauaji ya George Floyd

Wazungu wajionao bora (White Supremacists) wameyatafsiri machafuko ya kibaguzi yaliyojiri kufuatia mauaji ya Mmarekani mweusi George Floyd ambayo yalifanywa na askari polisi mzungu mwaka 2020, kuwa ni ishara ya kutoweka utambulisho wa Marekani, na kwamba inapasa wao wabebe silaha kuzuia jambo hilo lisitokee. Mtazamo huo wa kufurutu mpaka na utumiaji nguvu wa makundi ya ubaguzi wa rangi ya Wazungu wajionao bora yamekabiliwa na jibu la utumiaji nguvu pia la baadhi ya makundi yanayopiga vita Ufashisti kama Antifa. Kwa maneno mengine ni kuwa, Marekani, sasa imeingia kwenye awamu mpya ya mzunguko wa kujirudia, wa machafuko ya ubaguzi wa rangi; ambapo utumiaji nguvu wa kundi moja unaibua machafuko na utumiaji mkubwa zaidi wa mabavu wa kundi jengine, mwenendo ambao makamu wa rais wa nchi hiyo ameutaja kuwa ni "ueneaji chuki wa nchi nzima."

Pamoja na yote hayo, taasisi yenyewe ya serikali na vyombo vya kulinda usalama na vya sheria vya Marekani, huwa mara nyingi vinashadidisha migongano hiyo ya kijamii; na kutokana na kauli na hatua zao huwa kama wanamimina petroli kwenye moto uwakao, kiasi cha kuwafanya baadhi ya wanafikra wa nchi hiyo watoe indhari kwamba, isipotafutwa njia ya kulitatua janga lililopo si hasha Marekani ikakumbwa na vita vya pili vya wenyewe kwa wenyewe, ambavyo vinaweza vikasababisha maafa na uharibifu mkubwa zaidi kuliko wa vita vya kwanza vilivyotokea katikati ya karne ya 19.../