May 17, 2022 03:04 UTC
  • Marekani na NATO zafanya mazoezi ya kijeshi karibu na mipaka ya Russia

Mazoezi ya kijeshi ya pamoja baina ya Marekani na Jeshi la Nchi za Magharibi NATO yanaendelea hivi sasa katika ardhi ya Estonia, karibu na kambi za kijeshi za Russia.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, luteka hiyo imepewa jina la "Nungunungu 10" na inazishirika pia nchi za eneo hilo kama Finland na Sweden ambazo zinatarajiwa kupewa uwanachama rasmi wa NATO katika kipindi cha siku chache zijazo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, maneva hayo ya kijeshi ya NATO katika mipaka ya Russia yamepangwa kufanyika hadi tarehe 3 mwezi ujao wa Juni.

Jeshi la Nchi za Magharibi NATO limetangaza kuwa, lengo la mazoezi hayo ya kijeshi ni kujiweka tayari na kupima uwezo wa ushirikiano wa nchi wanachama. Karibu wanajeshi 15,000 wanashiriki kwenye luteka hiyo ambayo inahesabiwa ni kubwa zaidi kuwahi kufanywa na NATO tangu mwaka 1991.

Sehemu ya mazoezi ya kijeshi ya NATO na Marekani nchini Estonia karibu na mipaka ya Russia 2022

 

Mazoezi hayo ya kijeshi ya nchi za Magharibi yanafanywa katika eneo lililoko umbali wa kilomita 64 kutoka kwenye kambi ya Russia na wataalamu wanasema kuwa, lengo lake hasa ni kujaribu kujipima nguvu zao nchi za Magharibi za kukabiliana na mashambulizi ya Russia, iwapo Moscow itaamua kuanzisha vita dhidi ya Estonia. 

Russia inasema kuwa, Jeshi la Nchi za Magharibi NATO ni tishio kwa usalama wake na muda wote imekuwa ikizionya nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani, zisifanye uchokozi kwenye mipaka ya Russia kwani madhara yake ni makubwa na hayatabiriki. Hata hivyo nchi za Magharibi zinaoenakana "vichwa ngumu" na zinaonesha kutoshughulishwa na wasiwasi huo wa Russia.

Tags