May 17, 2022 11:32 UTC
  • Lavrov: Nchi za Magharibi zimehodhiwa na kudhibitiwa na Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergey Lavrov, ametahadharisha kuhusu uamuzi ilioamua kuchukua Sweden wa kujiunga na shirika la kijeshi la NATO na kueleza kwamba nchi za Magharibi zimehodhiwa na kudhibitiwa na Marekani.

Takriban miezi mitatu imepita tangu vilipoanza vita vya Ukraine, na hadi sasa nchi 25 zimeshaipatia nchi hiyo silaha na zana kivita za aina mbalimbali. Russia imekuwa ikisisitiza kuwa haina nia ya kuikalia kwa mabavu ardhi ya Ukraine.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, Lavrov amebainisha kuwa, shirika la kijeshi la NATO limehalifu ahadi yake ya kutoipatia silaha Ukraine na kutohatarisha usalama wa nchi zingine; na matokeo yake ni kushuhudiwa kujipanua kiholela na kusio na mipaka kwa shirika hilo la kijeshi la Magharibi kuelekea mashariki ya Ulaya.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameendelea kueleza kwamba, Marekani imezihodhi na kuzidhibiti nchi za Magharbi na akaonya kwa kusema, Moscow inafuatilia kwa makini harakati za NATO katia ardhi za nchi za Sweden na Finland.

Wakati huohuo msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov ameeleza kuwa Marekani, ni nchi mpenda uhasama na akafafanua kwa kusema: "Kuwepo kwa Russia kunaiudhi Marekani; na Marekani na waitifaki wake wa Magharibi ndani ya NATO wanafanya kila wawezalo ili kuzuia maendeleo ya Russia, lakini sisi tuna uhakika kuwa tutashinda na kufikia malengo yetu."

Hayo yanabainishwa katika hali ambayo waziri wa mambo ya nje wa Sweden Ann Linde ametangaza kuwa ameshasaini barua ya ombi la nchi yake kujiunga na shirika la kijeshi la NATO na amelitaja tukio hilo kama siku ya kihistoria kwa nchi hiyo ya Ulaya.../