May 17, 2022 11:40 UTC
  • Mbunge Muislamu awasilisha mpango wa kutambuliwa Nakba katika bunge la Marekani

Rashida Tlaib, mbunge Muislamu mwenye asili ya Palestina katika Kongresi ya Marekani amewasilisha kwenye bunge la nchi hiyo mpango wa kutaka kutambuliwa "Siku ya Nakba".

Siku ya Nakba kwa Wapalestina ni siku katika mwezi Mei 1948, ambapo zaidi ya robo tatu ya eneo la kihistoria na la asili la ardhi ya Palestina lilipovamiwa na kukaliwa kwa mabavu, Wapalestina 531 walipouliwa; na kufukuzwa na kugeuzwa wakimbizi karibu asilimia 85 ya idadi ya watu wa Palestina waliolazimika kukimbilia nchi jirani ikiwemo Jordan, Syria, Lebanon na baadhi ya nchi nyingine za nje ya Ukanda wa Asia Magharibi, kama inavyoeleza ripoti ya idara kuu ya takwimu ya Palestina.

Rashida Tlaib, mwakilishi wa jimbo la Michigan katika Baraza la Wawakilishi la Marekani ameeleza katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa Twitter kwamba, amewasilisha kwenye baraza hilo mpango kuhusu Siku ya Nakba kwa ushirikiano na uungaji mkono wa wabunge wenzake kadhaa jana Jumatatu, siku moja baada ya Wapalestina kuadhimisha mwaka wa 74 wa tukio hilo chungu la maafa ya kulazimishwa kuhama katika makazi yao ya asili sambamba na kuasisiwa utawala bandia na haramu wa Israel.

Katika ujumbe wake huo, Tlaib amebainisha kuwa, "leo nimewasilisha mpango wa kutaka kutambuliwa Nakba; siku ambayo miji na vijiji 400 vya Palestina vilibomolewa; na zaidi ya Wapalestina laki saba walihamishwa katika nyumba zao na kuwa wakimbizi."

Japokuwa ni baidi kwamba mpango huo utaweza kupitishwa katika Baraza la Wawakilishi la Marekani linalohodhiwa na waungaji mkono wa utawala haramyu wa Kizayuni wa Israel, lakini watetezi wa haki za Palestina wameitaja kuwa ni ya "kihistoria" hatua hiyo iliyochukuliwa na Rashida Tlaib, ambaye amewasilisha mpango huo kwa ushirikiano na uungaji mkono wa wabunge wenzake kadhaa ambao ni Betty McCollum, Marie Newman, Ilhan Omar na Alexandria Ocasio-Cortez.../