May 18, 2022 12:49 UTC
  • WMO: Joto linaendelea kuongezeka duniani kwa mwaka wa saba mfululizo

Shirika la Umoja wa Mataifa la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani, WMO limetangaza kuwa, hali ya hewa inaendelea kuwa mbaya duniani licha ya wadau kujadiliana kila uchao na kuahidi kuchukua hatua madhubuti za kulinda dunia kutoathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi ambayo kwa kiasi kikubwa yanaathiriwa na shughuli za kibinadamu.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa leo na WMO, shirika hilo la UN limepima viashiria vinne muhimu vya kuonesha mabadiliko ya hali ya hewa duniani ambavyo ni kiwango cha gesi chafuzi katika tabaka la ozoni, kupanda kwa kina cha bahari, joto la bahari pamoja na asidi ya bahari kuongezeka; na kwa mujibu wa ripoti yake hiyo WMO imethibitisha kuwa mwaka 2021, ukiwa ni mwaka wa saba mfululizo, kumekuwa na ongezeko la joto duniani.

Wastani wa joto lililoongezeka mwaka uliopita wa 2021 umeelezwa kuwa ni 1.11, hii ikimaanisha kuwa ni sawa na ongezeko la nyuzi joto 0.13 katika Selsiyasi juu ya kiwango cha kawaida, huku sababu kubwa ikielezwa ni tukio la Nina mwanzoni na mwishoni mwa mwaka 2021.

Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la utabiri wa hali ya hewa duniani Profesa Petteri Taalas amesema, kwa hali ilivyo sasa ni lazima dunia ichukue hatua katika muongo huu ili kuzuia athari za hali ya hewa zinazozidi kuwa mbaya na kuweka ongezeko la joto hadi chini ya nyuzi joto 1.5 katika selsiyasi.

Petteri Taalas

“Hali ya hewa inabadilika mbele ya macho yetu, ni suala la muda kabla hatujaona mwaka mwingine wenye joto zaidi katika rekodi," ameeleza Prof. Taalas.

Katibu Mkuu huyo wa WMO amefafanua kuwa, kupanda kwa kina cha bahari, joto la bahari kuongezeka na kuongezeka kwa chumvi baharini kutaendelea kuwa na athari kwa mamia ya miaka, iwapo hatua za haraka hazitabuniwa za kusaidia kupunguza uharibifu wa tabaka la ozoni; na kwamba mpaka sasa athari zinazidi kushamiri ulimwenguni, akitolea mfano zaidi ya watu bilioni mbili ambao tayari wana shida ya maji.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameitumia ripoti hiyo ya WMO kutoa mwito wa kuchukuliwa hatua ya kutumia nishati jadidifu na kupendekeza hatua kadhaa muhimu za kuchukuliwa ili kuanza kwa mpito matumizi ya nishati hiyo mbadala.../ 

Tags