May 18, 2022 14:50 UTC
  • COVID-19 imeua Wamarekani milioni moja hadi sasa

Marekani imekuwa nchi ya kwanza duniani ambayo idadi ya raia wake waliopoteza maisha kutokana na COVID-19 imepindukia milioni moja.

Kwa mujibu wa data zilizokusanywa na Chuo Kikuu cha John Hopkins, Marekani ni nchi iliyoathiriwa vibaya zaidi na COVID-19 duniani ambapo watu milioni moja wamefariki kutokana na ugonjwa huo ulioripotiwa kwa mara ya kwanza duniani mwishoni mwa mwaka 2019.

Ingawa vifo vimepungua katika wiki za hivi karibuni lakini wanaofariki kutokana na COVID-19 nchini Marekani ni takribani watu 360 kwa siku.

Vifo vitokanavyo na COVID-19 nchini Marekani sasa ni zaidi ya watu waliopoteza maisha kutokana na Ukimwi nchini humo. Itakumbukwa kuwa mwanzo wa maambukizi ya COVID-19 rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump aliudharau sana ugonjwa huo huku akijigamba kuwa vifo havitazidi watu laki moja.

Ubaguzi mkubwa katika sekta ya afya Marekani umetajwa kuwa moja ya sababu ya vifo vingi kutokana na COVID-19. Baadhi ya takwimu zinaonyesha kuwa Wamarekani wenye asili ya Afrika wameathiriwa vibaya na COVID-19. Uchunguzi umebaini kuwa katika kila Wamarekani laki moja wenye asili ya Afrika 344 wamepoteza maisha kutokana na COVID-19.  Taarifa zinaonyesha kuwa katika baadhi ya mitaa, jamaa wa familia nzima za Wamarekani wenye asili ya Afrika wameaga dunia kutokana na COVID-19.

Kaburi la umati kwa walipoteza maisha kutokana na COVID-19 nchini Marekani

Marekani imekumbwa na masaibu hayo wakati ilitumia janga la COVID-19 kuziadhibu nchi mahasimu wake kama Iran kupitia vikwazo. Marekani iliweka vikwazo vingi sana ili kuzuia Iran isipate uwezo wa kununua dawa na vifaa vya kukabiliana na COVID-19. Hatahivyo  Iran ilibadilisha vikwazo hivyo na kuwa fursa ya kujitosheleza katika sekta ya afya na ikaweza kujitengenezea dawa za kukabiliana na COVID-19 na pia aina kadhaa za chanjo. Hivi sasa  maambukizi ya COVID-19 nchini Iran yamefika kiwango cha chini kabisa huku zoezi la chanjo likiendelea kwa kutegemea chanjo zilizotengezwa nchini.