May 19, 2022 02:12 UTC
  • Vigezo vya nyuso mbili vya nchi za Ulaya katika suala la wakimbizi

Huku mgogoro wa kiuchumi na kisiasa ukiendelea katika baadhi ya nchi za Asia na huku vita baina ya Ukraine na Russia navyo vikiendelea, wimbi la wakimbizi katika mipaka ya nchi za Ulaya nalo limeongezeka.

Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu pamoja na lile la Hilali Nyekundu yametoa mwito kwa nchi nchi za Ulaya kutofanya ubaguzi katika kadhia ya wakimbizi. Mashirika hayo yamesema, hatua ya nchi za Ulaya ya kuwapokea haraka wakimbizi wa Ukraine haiendani kabisa na siasa kali za nchi hizo ambazo zinawazuia wakimbizi wa maeneo na mataifa mengine kuingia kwenye ardhi za nchi za Ulaya.

Siasa za kibaguzi na unyanyasaji za nchi za Magharibi dhidi ya wakimbizi wa nchi za Afrika na Kiarabu kama Palestina, Syria, Iraq na Yemen pamoja na wakimbizi wa maeneo mengine ya Asia Magharibi zimekuwa zikilalamikiwa vikali na duru mbalimbali ulimwenguni. Nchi za Magharibi zinawanyanyapaa na zinafuata siasa za ukandamizaji na za kuwarudisha walikotoka au kuwahamishia nchi nyingine wakimbizi hao kiasi kwamba takwimu za Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, wakimbizi wengi wa Afghanistan, katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni na ambao walikimbia nchi yao baada ya kuingia madarakani kundi la Taliban, si tu wametelekezwa na nchi za Magharibi na Marekani, lakini pia hata wale waliofanikiwa kuingia kwenye nchi za Magharibi wanaishi katika mazingira magumu sana kwenye kambi za wakimbizi. Hii ni katika hali ambayo, baada ya kupita takriban miezi mitatu ya vita vya Ukraine sehemu kubwa ya wakimbizi wa nchi hiyo wamepokewa kwa shangwe na nchi za Magharibi. Takwimu hizo zinaonesha kuwa, zaidi ya wakimbizi milioni tano wa Ukraine walioikimbia nchi hiyo baada ya kuanza vita, sehemu yao kubwa tayari wameshapewa hifadhi katika nchi za Ulaya.

Wakimbizi wa Ukraine

 

Ylva Johansson, kamishna wa masuala ya ndani ya Umoja wa Ulaya amesema, mazingira ya kupokea wakimbizi wa Ukraine barani humo yanatofautiana kabisa na mazingira ya wakimbizi wa eneo la Asia Magharibi kiasi kwamba hivi sasa nchi za Umoja wa Ulaya hata zimetangaza nafasi pana zaidi ya kupokea wakimbizi wa Ukraine tofauti na wakimbizi wa maeneo mengine.

Siasa za nyuso mbili za nchi za Ulaya zinaendeshwa katika hali ambayo tofauti kabisa na madai yao ya kupigania haki za binadamu, nchi hizo za Ulaya zinaonesha wazi kuwa hazishughulishwi hata kidogo na haki hizo za binadamu. Sasa hivi wakimbizi wengi wa nchi nyingine wanateseka katika mipaka ya nchi za Ulaya  na wengine wengi wanaishi kwenye kambi za wakimbizi kwa suhula chache mno za kumuwezesha mwanadamu kuishi. Hayo ni katika hali ambayo nchi za Magharibi, za Ulaya na Marekani ndio wasababishaji wakuu wa kuweko wimbi hilo la wakimbizi duniani. 

Kwa upande wake, Filippo Grandi, Katibu Mkuu wa Masuala ya Wakimbizi wa Umoja wa Mataifa ameonya kuhusu kuongezeka mateso na ukandamizaji wanaofanyiwa wakimbizi na wahajiri katika mipaka ya nchi za Ulaya na kusema kuwa, tunachokishuhudia hivi sasa kwenye mipaka ya nchi za Ulaya hakikubaliki kabisa; kisheria na kimaadili na inabidi kikomeshwe mara moja.

Filippo Grandi, Katibu Mkuu wa Masuala ya Wakimbizi wa Umoja wa Mataifa

 

Kama tulivyosema hivi punde, nchi za Ulaya zinawakandamiza wakimbizi wa maeneo mengine katika hali ambayo nchi hizo za Magharibi pamoja na Marekani ndizo zilizowalazimisha watu hao wakimbie maeneo yao na wawe wakimbizi. Ni jambo lililo wazi kwamba, hakuna mtu anayependa kukimbia nchi yake, lakini siasa za kiuadui na kibeberu za nchi za Magharibi ndizo hasa zilizozusha vita na machafuko katika maeneo tofauti duniani kiasi kwamba hata katika suala la vita vya Russia na Ukraine pia, wachochezi wakubwa wa vita hivyo ni nchi za Ulaya na Marekani na ndizo zinazovishadidisha.

Siasa za nyuso mbili za nchi za Magharibi hazionekani tu katika kadhia ya wakimbizi, bali katika upande wa vita vya Ukraine na Russia pia, nchi hizo zinafuata siasa za kindumilakuwili kikamilifu. 

Yulia Sveshnikova, Mshauri wa Taasisi ya Utafiti wa Kisiasa ya Russia ambaye pia ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nottingham anasema: Vigezo hivyo vya nyuso mbili si siasa ambazo zilianza baada ya kuanza vita vya Ukraine bali hizo ndizo siasa hasa na za wazi za nchi za Magharibi.

Tags