May 19, 2022 02:30 UTC
  • Russia: Hatutoruhusu kutokea Vita vya Tatu vya Dunia

Naibu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia amesisitiza kuwa, Moscow haitoruhusu kutokea Vita vya Tatu vya Dunia.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Dmitry Medvedev ambaye pia alikuwa Rais wa Russia kuanzia mwaka 2008 hadi 2012 amesema hayo wakati alipotembelea kituo cha nyuklia cha Shirikisho la Russia na kuongeza kuwa, kituo hicho kitaendelea daima kuwa kumbukumbu ya watu waliojitolea kila kitu chao kwa ajili ya kuifanya Russia kuwa dola lenye nguvu za nyuklia.

Naibu huyo wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia pia amesema, silaha za kisasa, za kutegemewa na zenye taathira kubwa, zinatosha kuvunja tabia ya kupenda makuu watu ambao wako tayari kuitumbukiza dunia kwenye vita vya tatu vikuu.

Nguvu za kijeshi za Russia

 

Amesisitiza kuwa, kamwe Russia haitoruhusu kutokea vita hivyo na kuongeza kuwa, pamoja na kwamba huo ndio msimamo usioyumba wa Moscow lakini inabidi tukumbushe muda wote kwamba, tutajibu haraka mno na vikali sana shambulio lolote lile litakalofanywa dhidi ya nchi yetu.

Aidha amezionya nchi za Magharibi na Marekani kwa kuendelea kupenyeza silaha ndani ya Ukraine kwa mgongo wa Jeshi la Nchi za Magharibi NATO na kusema kuwa, kitendo hicho cha nchi za Ulaya na Marekani kinaweza kuitumbukiza dunia kwenye vita vikubwa na vya pande zote vya nyuklia.

Dmirty Medvedev pia amesema, Moscow itatumia silaha zake za nyuklia katika hali nne tu na moja ni iwapo Russia itashambuliwa au iwapo muitifaki wa Russia atashambuliwa kwa kiwango cha kuhatarisha usalama wa kitaifa wa nchi hiyo.