May 19, 2022 07:10 UTC
  • Guterres: Karibu watu bilioni 2.2 hawana maji safi ya kunywa duniani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kwamba, kati ya kila watu watatu duniani, zaidi ya mtu mmoja hana maji safi ya kunywa na hiyo ni sawa na karibu watu bilioni 2.2 ulimwenguni.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, António Guterres alisema hayo jana Jumatano katika kikao cha mawaziri wa afya na maji na huku akigusia hali hiyo ya kutisha ya karibu watu bilioni 2.2 kutokuwa na maji safi na salama ya kunywa  amesema, watu milioni 884 hawana hata huduma za chini kabisa za maji safi ya katika kona mbalimbali za dunia.

Amesema, karibu watu bilioni 4.2 hawana huduma za kuaminika za afya na inakadiriwa kuwa, watu bilioni 3 duniani wanaishi bila ya kuwa na suhula salama za angalau kuosha mikono yao.

António Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia amesema katika kikao hicho kwamba, bado anatoa mwito wa kufanyika juhudi kubwa zaidi za kuwafikisha maji salama ya kunywa watu wote duniani na kwenye vituo vyote vya huduma za afya ifikapo mwaka 2030. 

Mwezi Aprili mwaka huu pia, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema kuwa; takriban nusu ya idadi ya watu duniani hukumbwa na uhaba mkubwa wa maji kila mwaka.

Akizungumza katika Mkutano wa Nne wa Maji wa Asia na Pacific huko Japan na kuendelea , António Guterres alieleza kuwa: uhaba wa maji unadhoofisha haki za binadamu na kutishia usalama na amani. Alisema,,dunia inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa maji na malengo ya maendeleo endelevu hayajadiliwi tena hivi sasa.