May 19, 2022 10:30 UTC
  • Sisitizo la Ripota Maalumu wa UN kuwa vikwazo ni kinyume cha sheria; kashfa nyingine kwa Marekani

Ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa amesema vikwazo dhidi ya Iran ni ukiukaji wa haki za binadamu na kuitaka serikali ya Marekani iondoe vikwazo vyote dhidi ya watu wa Iran katika sekta za chakula, dawa maji na afya.

Profesa Alen Douhan, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa anayefuatilia taathira hasi za hatua za upande mmoja kwa haki za binadamu, Jumatano alizungumza na waandishi habari mjini Tehran na kutoa ufafanuzi kuhusu safari yake ya siku 12 nchini Iran ambayo pia ilijumuisha mikutano na maafisa mbali mbali nchini.

Amesema: "Kwa mtazamo wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Baraza la Haki za Binadamu hakuna chochote kinachoweza kuhalalisha vikwazo dhidi ya Iran. Vikwazo vya upande mmoja na vitisho vya kuweka vikwazo ni mambo ambayo yemehatarisha haki za binadamu nchini Iran. Vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Iran ambavyo vimeizuia nchi hii kuagiza bidhaa, vikwazo vya kibenki na vikwazo vya chakula na dawa vimepelekea kupungua pato la serikali na kuongezeka bei ya bidhaa ambapo miongoni mwa waliopata madhara ni watu masikini, wakimbizi na wanawake wajane wenye watoto."

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikikabiliwa na vikwazo mbali mbali vya kigeni tokea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979. Vikwazo hivyo vimekuwa katika sekta kama vile bishara ya kigeni, mafuta, huduma za kifedha na kibenki. Aidha mbali na vikwazo hivyo vya moja kwa moja Marekani imekuwa ikiweka vikwazo dhidi ya watu na mashirika ya kimataifa yanayofanya biashara na Iran. Vikwazo hivyo vimewaathiri wananchi kwani hata vinazuia dawa na huduma maalumu za kitiba kuingia nchini.

Vikwazo vina taathiri zilizo dhidi ya binaadamu na hilo haliwezi kufichika. Uchunguzi kuhusu vikwazo uliofanywa na Matthias Maucksch na  Florian Neumayr wataalamu wa uchumi na sheria za kimataifa unasema vikwazo dhidi ya nchi mbali mbali hupelekea kukosekana usawa, kuibuka umasikini na  kupungua ustawi wa pato halisi la nchi zilizolengwa.

Vikwazo ambavyo Marekani iliviweka dhidi ya nchi mbali mbali tokea mwaka 1991 hadi 2018 vilipelekea ongezeko la takribani asilimia 3.5 ya umasikini katika nchi zilizolengwa. Aidha ustawi wa pato halisi katika nchi zilizolengwa ulipungua kwa asilimia 2.

Iran ambayo ni moja ya nchi zilizowekewa kiwango cha juu zaidi cha vikwazo na Marekani, imepata hasara ya kibiashara na pia kiwango kikubwa cha fedha za nchi hii kimezuiwa nje ya nchi kutokana na vikwazo. Kwa mujibu wa Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa Profesa Alen Douhan vikwazo hivyo vimesababisha hasara ya dola bilioni 100 hadi 120 kwa uchumi wa Iran.

Javad Salehi Isfahani, mhadhiri wa masuala ya uchumi katika Chuo Kikuu cha Virginia anasema hivi kuhusu taathira ya vikwazo nchini Iran baina ya mwaka 2010 na 2019. "Familia za vijijini ndizo zilizopata pigo kubwa zaidi kutokana na vikwazo. Kuanzia mwaka 2020, umasikini katika maeneo ya vijiji uliongezeka mara mbili na katika miji kiwango hicho kilikuwa ni asilimia 60."

Ni wazi kuwa, vikwazo hivyo vilivyo kinyume cha sheria na vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Iran vimepelekea kuongezeka umasikini, mfumuko wa bei na mashinikizo ya kiuchumi dhidi ya wananchi.

Kwa msingi huo madai ya wanaoweka vikwazo kuwa vikwazo vyao haviathiri wananchi si ya kweli hata kidogo. Kwa hakika moja ya malengo ya Marekani katika kuiwekea Iran vikwazo shahidi ni kuhakikkisha wananchi wanapata shida kubwa ili kwa njia hiyo wawashinikize wakuu wa nchi.

Wataalamu wa masuala ya haki za binadamu katika uga wa kimataifa mnamo Okotoba 2021 walichapisha ripoti iliyoonyesha namna baadhi ya wagonjwa nchini Iran wameshindwa kupata dawa na vifaa vya tiba kutokana na vikwazo vya Marekani ambapo walisisitiza kuwa, vikwazo vya Marekani vimepelekea wagonjwa nchini Iran kutopata haki za kimsingi za binadamu hasa haki ya afya.

Watoto wenye ugonjwa wa ngozi kipepeo nchini Iran wamekosa matibabu kutokana na vikwazo vya Marekani

Vikwazo vya upande mmoja vya Marekani pia vimezuia mashirika ya kimataifa ya kutoa misaada kufikisha misaada na fedha nchini Iran; kwa msingi huo mashirika hayo yameshindwa kuwasaidia wakimbizi, hasa wakimbizi kutoka Afghanistan walioko nchini Iran. Hatua hiyo ya Marekani ni ukiukaji wa wazi wa haki za binaadamu na hii ni moja ya nukta zilizosisitizwa na Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika taarifa yake.

Ni kwa msingi huo ndio Ali Bahadori Jahrom Msemaji wa Serikali ya Iran akasema, kukiri Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuwa vikwazo vya upande mmoja vya Marekani ni kinyume cha haki za binadamu ni kashfa nyingine kwa serikali ya Washington ambayo imekuwa ikidai kuwa ni mtetezi wa haki za binadamu wakati inaendeleza mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Iran.