May 19, 2022 12:35 UTC
  • Amnesty International: Israel ikubali kubeba dhima ya jinai zake dhidi ya Wapalestina

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesisitiza kuwa, haipasi tusahau kuuawa kwa Shireen Abu Akleh, mwandishi wa habari wa televisheni ya Aljazeera.

Jumatano ya tarehe 11 Mei, askari wa utawala wa Kizayuni walivamia kambi ya wakimbizi Wapalestina ya Jenin katika Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan, ambako walimuua shahidi kwa kumpiga risasi, Shireen Abu Akleh, mwandishi wa habari wa televisheni ya Aljazeera alikuwa amevalia kizibao chenye alama ya mwandishi wa habari.

Shirika la Msamaha Duniani, Amnesty International limeeleza katika taarifa liliyotoa mapema leo kwamba, "Israel inapaswa ikubali kubeba dhima ya jinai zake dhidi ya Wapalestina na haipasi tusahau kuuawa kwa Shireen Abu Akleh, mwandishi wa habari wa televisheni ya Aljazeera."

Kabla ya hapo, shirika hilo la kutetea haki za binadamu lilisisitiza kuwa, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC inapasa ifungue njia kwa ajili ya kudhihirishwa wazi uadilifu na ukweli na kuhakikisha mwenendo wa kukwepa adhabu, ambao kuendelea kwake kunahamasisha utendaji jinai, unakomeshwa.

Wakati huohuo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi Wopke Hoekstra amesema, kuuawa kwa Shireen Abu Akleh ni tukio lenye kutia wasiwasi mkubwa na ametaka ufanyike uchunguzi mpana na wa wazi juu ya suala hilo.../

Tags