May 20, 2022 07:35 UTC
  • Marekani: Kiongozi wa Korea Kaskazini hana hamu yoyote ya kukutana na Biden

Jake Sullivan, mshauri wa usalama wa taifa wa serikali ya Marekani amesema, Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un ambaye hapo kabla aliwahi kukutana na kufanya mazungumzo na aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump, hajaonyesha hamu yoyote ya kukutana na rais wa sasa wa nchi hiyo Joe Biden.

Wakati Trump alipokuwa rais wa Marekani, Kim Jong Un alikutana naye mara mbili, ya kwanza ikiwa ni mwaka 2018 nchini Singapore, ambao ulikuwa mkutano wa kwanza kufanyika baina ya viongozi wa Korea Kaskazini na Marekani.

Katika kikao chao hicho, Trump na Kim walisaini taarifa ya pamoja iliyojumuisha baadhi ya mahakikisho ya kiusalama kwa Korea Kaskazini mkabala wa kutokomezwa silaha za atomiki katika rasi ya Korea.

Mkutano wa pili kati ya viongozi hao wawili ulifanyika Hanoi, Vietnam, 2019 ambapo Korea Kaskazini iliilalamikia Marekani kwa kutotekeleza ahadi ilizotoa katika kikao cha Singapore. Kwa sababu hiyo kikao hicho hakikuwa na tija na kikamalizika bila kufikiwa makubaliano yoyote.

Trump (kulia) alipokutana na Kim Jog Un

Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, Sullivan ametoa matamshi hayo akiwa ameandama na Biden katika ziara ya rais huyo wa Marekani nchini Korea Kusini hapo jana. Siku ya Jumapili, Biden anatazamiwa kuelekea Japan, na baadaye Australia na India ambako pia atakutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hizo.

Siku ya Jumatano, mshauri huyo wa usalama wa taifa wa rais wa Marekani alisema, upo uwezekano wa Korea Kaskazini kufanya jaribio la makombora ya balestiki au majaribio ya nyuklia sambamba na safari ya Biden nchini Korea Kusini.

Licha ya kuwekewa vikwazo kadhaa tangu mwaka 2006 baada ya kufanya jaribio lake la kwanza la silaha za atomiki, Pyongyang imekuwa ikisisitiza kuwa itaendelea kuimarisha uwezo wake wa kijeshi ili kukabiliana na vitisho vya kuwepo vikosi vya jeshi la Marekani katika eneo la rasi ya Korea.../

Tags