May 20, 2022 07:43 UTC
  • Taliban: Watangazaji wanawake wanapotangaza katika televisheni wafunike nyuso zao

Serikali ya muda ya Taliban nchini Afghanistan imetoa amri kwa watangazaji wanawake wanaofanya kazi katika chaneli za televisheni za nchi hiyo wafunike sura zao wakati wanapotangaza.

Katika agizo lake hilo jipya, serikali ya Taliban imezitaka chaneli zote za televisheni ikiwemo ya T'ulue News na chaneli zingine zenye uhusiano na televisheni hiyo, zihakikishe kuwa, kuanzia sasa watangazaji wote wanawake wanafunika sura zao wakati wanapoendesha vipindi vya televisheni.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wizara za kuamrisha mema na kukataza maovu na habari na utamaduni za serikali ya Taliban zimesisitiza kuwa amri hiyo imeshapitishwa na haiwezi kuhojiwa.

Inasemekana kuwa agizo hilo limefikishwa kwa vyombo vingine vyote vya habari vya taswira nchini Afghanistan.

Haibatullah Akhunzada

Kwa upande mwingine, mitandao ya kijamii imeonyesha picha za watangazaji wawili wanawake ambao wamevaa maski wakieleza kwamba, kwa amri ya wizara ya kuamrisha mema na kukataza maovu ya Taliban, kuanzia sasa watakuwa wanaonekana katika hali hiyo katika vipindi vya televisheni.

Kabla ya hapo, Kiongozi Mkuu wa Taliban nchini Afghanistan Haibatullah Akhunzada alitoa agizo lenye vipengee vinne la sheria mpya kuhusu mipaka ya vazi la Hijabu kwa wanawake wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa agizo hilo, wanawake wote wanalazimika kuvaa hijabu, ikiwemo kufunika nyuso zao wanapokuwa katika hadhara na kwamba watakaohalifu kufanya hivyo watachukuliwa hatua kali.../

Tags