May 20, 2022 08:10 UTC
  • Russia: Shirika

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia Maria Zakharova amegusia hatua ya shirika la kijeshi la NATO ya kutaka kuzipatia Finland na Sweden uanachama wa shirika hilo na akasema, shirika ambalo limekumbwa na "kifo cha ubongo" linahitaji kupatiwa viungo vipya.

Zakharova ameongeza kuwa, ni jambo la mantiki kwamba madamu NATO imekumbwa na "kifo cha ubongo" itahitaji haraka wachangiaji wa viungo (wanachama wapya); na akaashiria kauli iliyotolewa Novemba 2019 na rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, ambaye alisema shirika la kijeshi la NATO limekufa ubongo hivyo inapasa liandae manifesto ya stratejia mpya.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amebainisha kuwa, Paris imeunga mkono Finland na Sweden zipatiwe uanachama katika shirika la kijeshi la Nato; na akaongeza kwa kusema, kila kitu kiko wazi kabisa kulingana na mantiki ya Ikulu ya Elysee, kwamba shirika lililokufa ubongo linahitaji kupatiwa viungo vipya haraka.

Maria Zakharova

Siku ya Jumatano Finland na Sweden zilituma barua zao za maombi kwa Katibu Mkuu wa shirika la kijeshi la Nato Jens Stoltenberg kuomba kuwa wanachama wa shirika hilo.

Russia imeonya kuwa uamuzi huo uliochukuliwa na nchi hizo mbili wa kujiunga na shirika la kijeshi la Nato ni kosa kubwa na kwamba itachukua hatua kuhusiana na suala hilo.

Uanachama wa Finland na Sweden katika NATO unategemea ridhaa ya wanachama wote wa shirika hilo, ambapo hadi sasa Uturuki imetangaza kuwa inapinga wazo hilo ikisisitiza kuwa, kutokana na uwepo mkubwa wa makundi ya kigaidi katika ukanda wa Scandanavia, haikubaliani na wazo la kuzipatia nchi hizo mbili uanachama katika shirika la kijeshi la NATO.../

 

Tags