May 20, 2022 11:16 UTC
  • Ugonjwa  nadra wa monkeypox waenea Ulaya, Marekani

Huku dunia ikiwa bado inakabiliana na janga la COVID-19, maambukizi ya kirusi nadra cha monkeypox yameripotiwa Ulaya na Marekani na kupelekea hali ya tahadhari ya kiafya kutangazwa.

Hadi kufikia sasa kumeripotiwa kesi 68 za monkeypox katika nchi kama vile Uingereza, Ureno, Marekani, Canada na Ausralia.

Monkeypox husababishwa na virusi vya monkeypox, kirusi cha familia moja ya virusi vya ndui, ingawa sio kali sana na wataalamu wanasema uwezekano wa kuambukizwa ni mdogo.

Inatokea zaidi katika sehemu za nchi za Afrika ya kati na magharibi, karibu na misitu ya kitropiki. Kesi ya kwanza ya ugonjwa huu iliripotiwa kwa mara ya kwanza huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika miuongo wa 70

Kuna aina mbili kuu za virusi - Afrika Magharibi na Afrika ya Kati. Dalili za awali ni pamoja na homa, kuumwa na kichwa, uvimbe, maumivu ya mgongo, kuumwa misuli na udhaifu wa mwili kwa ujumla.

Mara baada ya homa, upele unaweza kutokea, mara nyingi huanzia kwenye uso, kisha kuenea katika sehemu nyingine za mwili, kwa kawaida viganja vya mikono na nyayo za miguu. Upele, ambao unaweza kuwasha sana, hubadilika na kupita hatua tofauti kabla hatimaye kutengeneza kipele, ambacho hutumbuka baadaye.

Vidonda vinaweza kusababisha makovu. Monkeypox inaweza kuambukizwa wakati mtu yuko karibu na mtu aliyeambukizwa. Virusi vinaweza kuingia mwilini kupitia ngozi iliyo na jeraha au michubuko, kwa njia ya upumuaji au kupitia macho, pua au mdomo. Inaweza pia kuenezwa kwa kugusana na wanyama walioambukizwa kama vile nyani, panya na kindi, au kwa vitu kama vile matandiko na nguo. Maambukizi kwa kawaida huishia kwenye yenyewe na hudumu kati ya siku 14 hadi 21.

Shirika la Afya Duniani lilitoa taarifa Jumatano na kusema maambukizi yameanzia nchini Uingereza. Mtaalamu wa epidemolojia kutoka Uingereza Mateo Prochazka amesema baadhi ya watu wameambukizwa monkeypox nchini humo kupitia uhusiano wa kijinsia na kuongeza kuwa jambo hilo litakuwa na taathiria katika kukabiliana na kudhibiti kirusi hicho.