May 20, 2022 11:21 UTC
  • UN: Njaa itaziathiri nchi zote duniani, Iran yaahidi kusaidia 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba vita vinapozuka, watu hukabiliwa na njaa, na kwamba asilimia 60 ya watu wasio na lishe bora duniani wanaishi katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro huku akikumbusha kuwa "Hakuna nchi iliyo na kinga dhidi ya njaa,"  

Akizungumza  katika mkutano wa Baraza hilo mjini New York Marekani kuhusu migogoro na uhakika wa chakula Antonio Guterres amesema mwaka jana, asilimia kubwa ya watu milioni 140 wanaokabiliwa na njaa kali duniani kote waliishi katika nchi kumi tu ambazo ni Afghanistan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Ethiopia, Haiti, Nigeria, Pakistan, Sudan Kusini, Sudan, Syria na Yemen na kwamba nchi nane kati ya nchi hizi ziko kwenye ajenda ya Baraza la Usalama 
Ameongeza kuwa, “Ni bayana kwamba Baraza hili linapojadili migogoro, mnajadili njaa, mnapofanya maamuzi kuhusu ulinzi wa amani na operesheni za kisiasa, mnafanya maamuzi kuhusu njaa. Na mnaposhindwa kufikia muafaka, watu wenye njaa hulipa gharama kubwa,”  
Guterres amesema mgogoro wa Ukraine pia umechochea tatizo la njaa akilikumbusha Baraza kuwa “Hadi mwezi Machi mwaka huu Ukraine ilikuwa inailisha dunia kwa chakula chake kingi lakini sasa inategemea msaada wa chakula ambapo mwezi Aprili shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP liligawa chakula kwa zaidi watu milioni 3 nchini Ukraine.” 

Antonio Guterres

Pia amesema anatiwa hofu na changamoto ya kutokuwa na uhakika wa chakula Pembe ya Afrika kutokana na ukame ambao haujawahi kushuhudiwa kwa takriban miongo minne. Watu milioni 18 wameathirika huku WFP ikionya kwamba mathalani Somalia mamilioni ya watu wako kwenye hatihati ya baa la nja katika miezi michache ijayo. 

Duniani kote watu milioni 49 katika nchi 43 wako kwenye kiwango cha hatari na cha dharura cha njaa huku waathirika wakubwa wakiwa ni wanawake, wasichana na watoto na vita vya Ukraine vimezidisha madhila 

Wakati huo huo akihutubu katika kikao hicho cha Baraza la Usalama, Majid Takht-Ravanchi Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema dunia nzima sasa inakabiliwa na uhaba wa chakula na kuongeza kuwa: “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono jitihada za Umoja wa Mataifa za kutatua matatizo ya ukosefu wa chakuka duniani. Aidha amesema uwepo wa mamilioni ya wakimbizi kutoka nchi jirani ya Afghanistan ni jambo ambalo limezidisha mashinikizo katika uchumi wa Iran na ni mzigo kwa usalama wake wa chakula.