May 21, 2022 03:14 UTC
  • Uungaji mkono wa Iran kwa hatua za Umoja wa Mataifa katika kukabiliana na mgogoro wa chakula duniani

"Dunia nzima imeathirika na uhaba wa chakula." Hayo yalisemwa siku ya Alhamisi na Majid Takht-e Ravanchi, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa.

Akizunumza karibuni katika kikao cha Baraza la Usalama kilichofanyika chini ya anwani ya "Ukosefu wa Usalama wa Chakula na Migogoro," Takht-e Ravanchi alisema: "Mabadiliko ya hali ya hewa, janga la Covid-19 na athari hasi za migogoro ya kimataifa, yote hayo yameziathiri nchi nyingi, ikiwemo Iran ambayo imekabiliwa na vikwazo vya Marekani kwa zaidi ya miongo minne."

Matamshi ya Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa kuhusu mzozo wa chakula duniani kutokana na hali isiyokuwa ya kawaida ya uhaba wa bidhaa za kimkakati za chakula kama vile ngano, mahindi na mbegu za mafuta kutokana na vita vya Ukraine yanaweza kufahamika vyema kupitia tathmini ya vita vya Ukraine na taathira zake hasi katika uzalishaji na mauzo ya nje ya bidhaa hizo katika nchi mbili kuu wazalishaji, yaani Russia na Ukraine. Nchi mbili hizo kwa pamoja zinazalisha takriban asilimia 30 ya ngano na karibu asilimia 80 ya mbegu za mafuta ulimwenguni, nyingi zikiwa zinatumwa katika mataifa ya Afrika na Asia Magharibi. Russia ni mojawapo ya nchi zinazouza kwa wingi mbolea za kemikali duniani, na hivyo vikwazo vikubwa vya nchi za Magharibi kwa nchi hiyo vimesimamisha usafirishaji wa bidhaa hiyo muhimu kwa sekta ya kilimo duniani.

Takht-e Ravanchi, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa

Qu Dongyu, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ameashiria ongezeko kubwa la bidhaa za chakula katika siko la kimataifa na kusema: "Russia na Ukraine ni wahusika muhimu katika soko la kimataifa la nafaka, na vita kati ya nchi hizo mbili imekuwa sababu muhimu ya kuongezeka bei ya chakula duniani, hasa ngano, mahindi na mbegu za mafuta. Ongezeko hilo limetokea huku mahitaji ya bidhaa hizi na gharama za uzalishaji zikiongezeka kufuatia kupungua kwa maambukizi ya corona."

Bila shaka, changamoto sugu kama vile mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yamebadilisha mfumo wa mvua na kuibua ukame wa muda mrefu katika sehemu mbalimbali za dunia zimeharibu zaidi mgogoro huo. Wakati huo huo, janga la corona limeathiri vibaya ukuaji wa uchumi wa nchi nyingi na hasa katika sekta ya uzalishaji na shughuli za kilimo. Aidha kupungua taratibu janga la Corona kumeongeza mahitaji ya chakula duniani. Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  amesema karibuni hivi katika kikao cha "Ongezeko la Mgogoro wa Chakula" kwamba: "Katika kipindi cha miaka miwili pekee, idadi ya watu wanaokabiliwa na uhaba wa chakula imeongezeka maradufu kutoka watu milioni 135 kabla ya janga hilo hadi milioni 276. Zaidi ya watu nusu milioni wanaishi katika hali ya baa la njaa, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 500 tangu 2016."

Hayo yote, pamoja na kudhihiri na kuendelea migogoro ya kieneo duniani hususan katika eneo la Magharibi mwa Asia ambako Iran pia inapatikana, kumesababisha suala la uhaba wa chakula kudhihirika zaidi katika eneo hili nyeti. Kuhusiana na hilo, Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema: Nchini Afghanistan, watu milioni 22 wanakabiliwa na uhaba wa chakula na wanahitajia sana msaada. Pia mwanzoni mwa mwaka huu wa 2022, uhaba mkubwa wa chakula nchini Yemen uliongezeka kwa asilimia 8% ya idadi ya watu waliokuwa katika shida ya uhaba wa chakula ikilinganishwa na mapema mwaka 2021. Hali ya kibinadamu nchini Palestina imezorota kutokana na miongo kadhaa ya kukaliwa kwa mabavu na kutekelezwa sera kandamizi za utawala wa kibaguzi wa Israel. Kwa upande wa Syria, kuendelea kukaliwa kwa mabavu ardhi ya nchi hiyo na askari wa kigeni, ugaidi na vikwazo vya upande mmoja kumesababisha mamilioni ya watu kuhama makazi yao na kuishi kama wakimbizi kwingineko, kuharibika maisha ya watu, kuvurugika biashara, chakula na kilimo, miundombinu na upatikanaji wa rasilimali muhimu kupungua.

Kikao cha FAO

Suala la mgogoro wa chakula duniani limepewa kipaumbele maalumu na Umoja wa Mataifa, ambapo taasisi pamoja na viongozi wa taasisi hiyo muhimu ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Katibu Mkuu wake, Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani ( FAO) wameonya kuhusu athari hasi za mgogoro huo. David Beasley, Mkurugenzi Mtendaji wa Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa amesema: "Sasa tunashuhudia kupanda kwa bei ya mafuta duniani; pia kuongeza bei ya chakula na usafiri. Suala hili sasa linasababisha machafuko, hasa kwa watu masikini duniani. Pamoja na hayo masuala haya hayaathiri watu maskini pekee." Akielezea hali ya usalama wa chakula duniani kutokana na vita vya Ukraine, Mkurugenzi Mkuu wa FAO anatabiri kuwa bei ya chakula duniani itaendelea kupanda katika miezi ijayo.

Tags