May 21, 2022 12:30 UTC
  • Askari laki moja wa Marekani kubaki Ulaya kwa kisingizio cha

Vyombo vya habari vya Marekani vimetangaza kuwa kuna uwezekano askari laki moja wa jeshi la nchi hiyo wakabaki barani Ulaya kwa ajili ya kukabiliana na kitisho cha Russia.

Televisheni ya CNN imezinukuu duru za kuaminika na kuripoti kuwa, wakati mivutano baina ya Magharibi na Russia juu ya mgogoro wa Ukraine ingali inaendelea, yamkini Washington ikawaweka kwa muda mrefu maelfu ya askari wake barani Ulaya kwa ajili ya kukabiliana na kile inachokiita "kitisho cha Russia".

Kwa mujibu wa maafisa wa Marekani ambao hawakutaka kutajwa majina yao, inategemewa kwamba Washington itaweka maelfu ya wanajeshi wake barani Ulaya kwa ajili ya mustakabali unaotarajiwa kushuhudiwa kwa sababu yamkini Russia ikashadidisha mivutano na kutoa vitisho kwa Sweden na Finland au wanachame wengine wa NATO.

Imeelezwa kuwa mipango hiyo ya Washington inatafakariwa kufuatia kikao cha siku ya Alkhamisi cha wakuu wa kijeshi wa nchi wanachama wa NATO kilichofanyika mjini Brussels.

Makamanda wa majeshi ya nchi wanachama wa Nato wanaandaa mapendekezo kwa ajili ya kikao cha mwezi ujao wa Juni cha mawaziri wa ulinzi wa muungano huo wa kijeshi wa Magharibi. Hayo yanajiri, huku viongozi wa nchi wanachama wa Nato akiwemo Rais Joe Biden wa Marekani wakitazamiwa kukutana mwishoni mwa mwezi huu mjini Madrid, Uhispania.

Kwa mujibu wa duru za kijeshi, kabla ya Russia kuishambulia kijeshi Ukraine, jumla ya askari 60 elfu wa jeshi la Marekani walikuwepo barani Ulaya; na hivi sasa idadi hiyo imeshaongezeka hadi kufikia askari wapatao laki moja.../