May 22, 2022 04:37 UTC
  • Hungary: Vikwazo dhidi ya Russia ni bomu la Atomiki

Waziri Mkuu wa Hungary amesema kuwa, vikwazo vya nchi za Ulaya na Marekani dhidi ya Russia ni sawa na bomu la nyuklia na vitazidisha njaa duniani na kuongeza wimbi la wakimbizi.

Viktor Mihály Orbán alisema hayo jana Jumamosi katika mazungumzo na waandishi wa habari aliyofanya kwa pamoja na Rais Aleksandar Vučić wa Serbia na kuongeza kuwa, sasa nchi zetu zinakabiliwa na kipindi cha baridi kali... vita vya Ukraine vimetuweka kwenye wakati mgumu. Jambo hilo ni zito sana kwetu kwa sababu nchi yetu ni mwanachama wa Umoja wa Ulaya lakini Hungary haikubali kutozingatia pande zote katika masuala yake ya kiuchumi. Haiwezi kufuata mkondo usioingia akilini wa Brussels dhidi ya Russia kwani utapandisha vibaya bei za bidhaa.

Wimbi la wakimbizi Ulaya Mashariki

 

Aidha amesema, hatupaswi kuweka vikwazo kwa pupa kwa sababu vikwazo dhidi ya Russia ni sawa na bomu la atomiki na ukweli ni kuwa kwa vikwazo hivyo, tutashindwa kuwadhaminia chakula watu wetu, lakini pia tutalazimika kupokea wakimbizi wengi zaidi katika mipaka yetu kwani njaa itakayosababishwa na vikwazo dhidi ya Russia itawafanya watu wakimbilie nchi nyingine na kuongeza sana wimbi la wakimbizi.

Vile vile amesema, mwaka 2020-2021 mashujaa wetu walikuwa ni watu wa afya waliopambana na UVIKO-19, mwaka huu mashujaa wetu watakuwa ni wakulima na ndio watakaotegemewa, tutake tukatae. Kwani kama chakula kitapotea dunaini watu watalazimika kuhama maeneo yao na watu hao si wale wanaotafuta maisha ya anasa, bali ni wale ambao wanapigania angalau kubakia hai na kupata japo kitu kidogo tu cha kuwawezesha kuendelea kuishi.