May 22, 2022 17:03 UTC
  • Maandamano ya kupinga safari ya Biden Korea Kusini

Wanachama wa baadhi ya vyama na mashirika ya kiraia wamekusanyika mjini Seoul kupinga ziara ya Rais Joe Biden wa Marekani nchini Korea Kusini.

Wapinzani wa ziara ya Rais wa Marekani nchini Korea Kusini wamekusanyika mitaani mjini Seoul wakiwa na mabango yenye maandishi yaliyosomeka: "Ziara ya Biden Korea Kusini yazidisha mgogoro wa vita", "tunapinga kuingia utawala wa Yoon Seok-youl katika vita baridi vya Marekani" na "tunapinga ushirikiano wa kijeshi kati ya Japan na Korea Kusini."

Waandamanaji wamesisitiza kuwa, sera ya kimsingi ya serikali ya Korea Kusini ya kuimarisha muungano wa kijeshi kati ya nchi hiyo na Marekani na wakati huo huo kuimarisha ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi mbili hizo na Japan, inazidisha mvutano wa kijeshi na mashindano ya silaha katika Peninsula ya Korea.

Maandamano ya watu wa Korea Kusini dhidi ya safari hiyo yamechochewa na uzoefu wa siasa za kichochezi za Ikulu ya White House katika Peninsula ya Korea, ambazo daima zimekuwa zikivuruga juhudi zinazofanywa na Korea mbili za kupunguza tofauti na kupanua ushirikiano kati yazo kwa shabaha ya kuleta utulivu katika eneo hilo.

Rais Joe Biden (kulia) akiwa ziarani Korea Kusini

Kwa kuzingatia kuingia madarakani rais mpya wa Korea Kusini na uwezekano wa kuwepo mabadiliko katika mikakati ya serikali yake, kuna wasiwasi miongoni mwa watu na mashirika ya kiraia ya Korea Kusini kwamba serikali hiyo mpya huenda ikatekwa na kutwishwa sera za White House katika kukabiliana na Korea Kaskazini. Wakorea wana wasi wasi kwamba siasa hizo za upande mmoja za White House ambazo zinalenga kulinda maslahi mahususi ya Marekani katika eneo hilo la Asia yanaweza kuzuia juhudi za utawala uliopita wa Seoul za kujaribu kuleta amani na utulivu kwa maslahi ya Korea mbili.

Kuna maoni kwamba lengo kuu la Biden katika safari yake huko Korea Kusini, mbali na masuala ya pande mbili, ni kujadili jinsi ya kuongeza mashinikizo dhidi ya Korea Kaskazini, jambo ambalo bila shaka litaongeza mvutano na ukosefu wa usalama katika Peninsula ya Korea.

Mashirika ya kiraia huko Korea Kusini yanamtaka rais mpya wa nchi hiyo apange sera za serikali yake kuhusu Korea Kaskazini kwa kuzingatia tu maslahi ya kitaifa na udharura wa kuwepo usalama na utulivu wa kikanda bila kujali mashinikizo ya Marekani, na wakati huo huo kuzuia wahusika wengine kuingilia masuala ya ndani ya eneo hilo.

Ziara ya Rais wa Marekani nchini Korea Kusini imeongeza uwezekano kwamba katika mazungumzo yake na mwenzake wa Korea, Rais wa Marekani atamtaka mwenyeji wake ashirikiane na Ikulu ya Marekani katika kuongeza mashinikizo dhidi ya Korea Kaskazini, jambo ambalo bila shaka litasababisha kushadidi migawanyiko na mivutano kati ya Korea mbili.

Katika kipindi cha utawala wa rais wa zamani wa Korea Kusini Moon Jae-in, jitihada zilifanyika kwa ajili ya kupunguza tofauti kati ya nchi hiyo na jirani yake Korea Kaskazini, lakini hujudi hizo hazikufranikiwa kutokana na vizingiti vilivyowekwa na Marekani.

Maandamano ya Wakorea Kusini dhidi ya safari ya Biden nchini humo

Serikali ya Marekani imeshurutisha makubaliano yoyote kati ya Korea mbili na kufikiwa mapatano kati ya Washington na Pyongyang kuhusu masuala ya nyuklia na makombora ya Korea Kaskazini, jambo ambalo linainyima Seoul fursa yoyote ya kupatana na jirani yake Korea Kaskazini.

Hasa tukitilia maanani kwamba, tangu kuanza duru ya kwanza ya mazungumzo kati ya Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un na Rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump huko Singapore mnamo Juni 2018, Washington imekuwa ikitekeleza sera zenye mgongano na haribifu dhidi ya Pyongyang, jambo ambalo lilimpelekea kiongozi huyo wa Korea Kaskazini kusitisha mazungumzo hayo mara tu baada ya kufanyika duru ya pili ya mazungumzo kati ya viongozi wa nchi mbili mnamo Februari 2019 huko Hanoi, mji mkuu wa Vietnam.

Tags