May 23, 2022 03:44 UTC
  • Wajapan waandamana mjini Tokyo kupinga safari ya Biden nchini mwao

Wananchi wa Japan wameandamana kupinga safari ya Rais Joe Biden wa Marekani mjini Tokyo.

Biden aliwasili mjini Tokyo jana akitokea Korea Kusini kuendelea na safari yake katika nchi kadhaa za Asia.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, mamia ya wananchi wa Japan jana waliandamana katika mji mkuu Tokyo kupinga safari ya Biden, ambaye anatazamiwa pia kushiriki kikao cha pande nne cha viongozi wa nchi wanachama wa QUAD, zinazojumuisha Japan, Marekani, Australia na India kitakachofanyika nchini humo.

Kufuatia safari hiyo ya Biden na kufanyika kwa kikao hicho, zaidi ya askari polisi na wa vikosi vya usalama elfu 18 wamewekwa katika hali ya tahadhari nchini Japan.

Aidha kwa mujibu wa mashuhuda, helikopta za polisi ya Japan zilikuwa zikipiga doria katika anga mji huo hapo jana.

Leo Biden anatazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo na waziri mkuu wa Japan Fumio Kishida; na kesho Jumanne atashiriki katika mkutano huo wa pande nne utakaohudhuriwa na mawaziri wakuu wa Japan, Australia na India.

Wananchi wa Japan kila mara wamekuwa wakipinga kuwepo askari wa Marekani na vituo vyake vya kijeshi katika ardhi ya nchi yao; na wameshaandamana mara kadha wa kadha kubainisha upinzani wao kwa serikali yao na kwa maafisa wa Marekani.

Halikadhalika, Wajapan bado hawajasahau kumbukumbu chungu ya mashambulio ya mabomu ya atomiki yaliyodondoshwa na Marekani mwaka 1945 katika miji ya Hiroshima na Nagasaki na kila mara wamekuwa wakibainisha chuki zao dhidi ya jinai hiyo ya kinyama iliyofanywa na Washington.../